17 September 2012

Unyanyapaa kikwazo mapambano ya VVU nchini



Na Agnes Mwaijega

KUKITHIRI kwa vitendo vya unyanyapaa na ubaguzi katika jamii yetu kumechangia kwa kiasi kikubwa kuharibu na kudhoofisha juhudi mbalimbali zinazofanywa kwa ajili kupambana na UKIMWI.

Pia unyanyapaa na ubaguzi hasa kwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi (VVU) ni miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele mara kwa mara hapa nchini na asasi za kiraia, wadau mbalimbali pamoja na serikali.

Hata hivyo pamoja na kwamba siyo wote wenye VVU wamevipata kwa kujitakia kupitia ngono zembe mpaka sasa bado tunashuhudia katika jamii yetu waathirika hawa wakitengwa na kufanyiwa vitu visivyofaa na vinavyowanyima  haki zao za msingi.

Baadhi ya haki za msingi pia zinakikukwa ikiwa ni pamoja na kukataliwa kurithi mali, kupigwa na kutengwa na wana jamii, watoto wanaoishi na VVU kukatazwa kucheza na watoto wasioishi na VVU, kutokupandishwa cheo kazini au kupewa madaraka mengine na kufukuzwa kazi.

Kwa mfano mfanyakazi aliyeambukizwa VVU kukoseshwa haki zake kwa kusimamishwa kazi, kutopandishwa cheo, au kuzuiliwa nafasi za mafunzo, pamoja na kutengwa na wafanyakazi wenzake.

Katika hudumza za afya wathirika wamekuwa wakitengwa  au kubugudhiwa kwa matusi na watoa huduma za matibabu, pia hudharauliwa wakati msaada wa huduma hiyo muhimu unapohitajika zaidi kwa hali yake.

Katika masuala ya kidini waathirika hao wanatazamwa kwa mtazamo hasi kwamba ni muasi hali inayosabanisha kunyimwa usirikiano.

Kwa upande wa shule waathirika hao wananyimwa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kujumuika na wenzao wanapokuwa katika mazingira ya shule.

Vile vile vitendo hivyo vimekuwa vikionekana katika familia ambapo waathirika wanatengwa na ndugu, jamaa na marafiki kwa kutazamwa vibaya na wakati mwingine kutohudumiwa.

Kutokana na vitendo hivyo imekuwa vigumu kwa waathirika kujitokeza hadharani ili kupata taaluma na njia za kujikinga, kutoa huduma kwa waathirika, matibabu au hatua za kupunguza  athari za milipuko yaa maradhi.

Matokeo yake ni kuongezeka kwa idadi ya waathirika na vifo vya wagonjwa wa UKIMWI kila mwaka jambo ambalo linahatarisha mustakabali wa taifa.

Kwa vile hali hii ya unyanyapaa na ubaguzi inaonekana kujikita kwa kiwango kikubwa katika jamii zetu, basi hatuna budi sote kwa pamoja kuungana kuitokomeza tabia hii ili mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo yaweze kupungua.

Hata hivyo inaeleweka wazi kwamba haki za binadamu zinaeleza kuwa ni lazima kuheshimu utu na thamani ya kila binadamu bila kujali anaishi au ameambukizwa VVU.

Kutokana na upeo mdogo juu ya masuala yanayohusu VVU kutokufahamu sheria na elimu ndogo ya haki za binadamu, watu wanaoishi na VVU na wagonjwa wa UKIMWI wamekuwa wakivunjiwa haki zao za msingi mara nyingi kuliko watu
wengine.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba dhana kubwa iliyojengeka katika jamii ni kuwa VVU, ni kifo na hakuna dawa ya VVU.

Hicho ndiyo chanzo kikubwa cha ukiukwaji wa haki za kibinadamu za watu wanaoishi na VVU na kutazamwa kwa mtazamo hasi.

Kwa sababu watu wanaoishi na VVU wanaonekana kama siyo wakamilifu tena katika jamii ndio maana hutengwa na kubaguliwa.

Mara nyingi hali hii hutokea hata kama walioambukizwa VVU bado wana afya zao na wanaweza kuzalisha mali katika jamii na kutunza familia zao bila kutegemea msaada wa mtu yeyote.

Mambo haya yanapotendeka katika jamii zetu watu wanaoishi na VVU hawawezi tena kufaidi haki zao za msingi kama watu wasio na VVU wanavyozifaidi.

Vitendo hivyo kama vilivyokithiri katika maeneo mengi nchini ndivyo ilivyo katika kata mbalimbali za Manispaa ya Wilaya ya Temeke.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Asasi ya Wajane Women Group (WWG) Bi.Dina Minja waathirika wa VVU katika kata hizo wanabaguliwa kunyanyapaliwa na wanajamii wanaowazunguka.

Wanakosa haki zao za msingi, hasa wanawake wamekuwa wakishuhudia jinsi wanavyofukuzwa na waume zao bila kupewa chochote.

Hali hiyo imesababisha waathirika wengi kujificha na kushindwa kujitokeza hadharani kupima ili waweze kupata matibabu au huduma za afya.

"Hali ya unyanyapaa katika jamii bado upo tena kwa kiasi kikubwa pamoja na kwamba serikali inapiga vita suala hilo," anasema.

Wapo wengi ambao baada ya kujitangaza wanajamii wanaowazunguka wamewatenga hali ambayo imesababisha kushindwa kuendelea na shughuli zao za maendeleo.

Anatoa mfano kwamba kuna mtu ambaye baada ya kupima na kujitangaza ndugu zake waliamua kumtenga kwa kumweka katika chumba cha peke yake bila kumpa msaada wowote.

Bi.Minja anasema kutokana na kukithiri kwa hali hiyo wameamua kutoa mafunzo ya athari za unyanyapaa ili wanajamii wote wawe na uelewa wa kutosha utakaoondoa fikra potofu.

Anaelezea kuwa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini yanakwamishwa kutokana na vitendo hivyo kwa sababu wengi wanalazimika kujificha kwa kuogopa kubezwa na kutengwa.

Waathirika wanajificha na inapofika wakati wanajitokeza na kujitambulisha hali zao zinakuwa tayari zimekuwa mbaya kwa sababu ya kuchelewa kuanza kupata huduma za kiafya.

Sababu kubwa ni ukosefu wa elimu na uelewa wa madhara ya vitendo hivyo ambavyo vinapaswa kupingwa vikali na kila mtanzania.

Anawashauri viongozi wa serikali, dini, wadau na watu mashuhuri kushirikiana na asasi za kiraia kutoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI na kushiriki kikamilifu katika kupambana na vitendo hivyo.

Mikakati ya itakayoweza kupunguza unyanyapaa na ubaguzi katika jamii iwekwe ikiwa ni pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu mambo ya msingi ya VVU, kwa kutumia njia za habari elimu na mawasiliano, kuanzisha na kuimarisha huduma za Unasihi katika vituo vyote vya Huduma

Kujenga mwamko, uhamasishaji miongoni mwa watoa huduma wa afya ili kuepuka vitendo au tabia za unyanyapaa, kutoa elimu endelevu kuhusu UKIMWI na unyanyapaa.

Watunga sera na viongozi wa Jamii waandae mipango madhubuti ihusuyo kinga na matunzo kwa WAVIU.

Kwa sababu Tanzania ni miongoni mwa nchi 189 wanachama wa Umoja wa Mataifa (AU) ambazo zimeahidi kutekeleza
malengo mbalimbali ya maendeleo ifikapo mwaka 2015 likiwemo lengo la 6.

Lengo ambalo linahimiza nchi wanachama kupambana na ugonjwa huo kwa kuzuia kabisa na kuanza kupunguza maambukizo mapya ya ukimwi.

Naye Bw.Martin Mbelwa anasema vitendo hivyo vinapaswa kupingwa kwa nguvu zote ili nchi iweze kufikia malengo yake.

Hata hivyo anatoa wito kwa waathirika kuacha kuogopa na kujiweka wazi ili waweze kuanza kupata huduma mapema.

Anasisitiza kuwa upo umuhimu wa kuhakikisha kuwa Watanzaia wote wanapewa elimu juu ya madhara yanayotokana na unyanyapaa na jinsi ya kuwasaidia waathirika.


No comments:

Post a Comment