17 September 2012
'Maadili ya dini yatumike kulea watoto'
Na Mariam Mziwanda
WITO umetolewa kwa wazazi nchini kuwalea watoto wao katika maadili yanayozingatia misingi ya dini badala ya kuwapa uhuru wa kutumia mitandao ya kijamii inayochangia wakose maadili.
Mkuu wa Shule ya Mtakatifu Theresa, iliyopo Ukonga, Bi. Amelberga Rwezahura, aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika maafali ya nane ya wanafunzi wa darasa la saba shuleni hapo.
“Wazazi tunachangia kuwaaribu watoto wetu, tunawapa uhuru wa kutumia mitandao ya kijamii ambayo inawafanya wajifunze mambo yasiyoendana na maadili ya Mtanzania,” alisema.
Alisema ili upo umuhimu wa watoto kuwekewa msingi mzuri wa maisha ya baadae kwa kuwalea katika maadili ya kiroho na kuhakikisha anapata elimu bora.
Aliongeza kuwa, wazazi nawapaswa kushirikiana na walimu kuhakikisha watoto wao wananufaika na elimu wanayopewa na kusisitiza kuwa, shule hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na wazazi ili malengo waliyonayo kwa watoto yaweze kufanikiwa.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali kupiga vita maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi, umaskini na kuleta maendeleo ya elimu kwa watoto nchini,” alisema.
Mgeni rasmi katika mahafali hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Uledi Mussa, mbali ya kuwasihi wazazi kusimamia malezi ya watoto, alitumia fursa hiyo kufanya harambee ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana shuleni hapo ili kuwaepusha na changamoto mbalimbali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment