10 September 2012

Rahma rais mpya CHANEZA



Na Mwajuma Juma, Zanzibar

MGOMBEA RAHMA Ali Khamis amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Chama Cha Mpira wa Netiboli Zanzibar (CHANEZA), baada ya kupata kura 30 kati ya 31 zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika Ecrotanal mjini Unguja.

Rahma ambaye ni Mkurugenzi wa  Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar katika Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana,
Wanawake na Watoto alichaguliwa kushika nafasi hiyo akiwa mgombea
pekee katika uchaguzi huo ambapo atakiongoza chama hicho kwa kipindi
cha miaka minne ijayo.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi, Kibabu
Haji Hassan kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abrahman Mohammed alisema  jumla ya wapiga kura wote walikuwa ni 31 na Rahma amepata kura 30 na kura moja iliharibika.

Aidha Kibabu alimtangaza Mkemimi Muhina Seif kuwa Makamu wa Rais
Unguja aliyepata kura 31 huku nafasi ya Makamu wa Rais Pemba
ikichukuliwa na Abdallah Suleiman Sharif aliyepata kura 21 na kumpita
mpinzani wake, Mwajuna Hija aliyepata kura 10.

Viongozi wengine waliochaguliwa ni Katibu Mkuu, Said Ali Mansab
aliyepata kura 23 na kuwapita wagombea wenzake, Subira Mohammed
aliyeambulia kura moja na Nasra Juma Mohammed aliyepata kura saba,
wakati wasaidizi wake wawili ni Bimkubwa Khamis Mohammed kura 19 kwa
Pemba na wa Unguja ni Saaduni Amed Abbas aliyepata kura 16.

Nafasi ya Mshika Fedha ilichukuliwa na Issa Mohammed Salum aliyepata
kura 26 na kumpita  mpinzani wake , Fedrick Michael Apyua
aliyepata kura tano wakati Msaidizi Mshika Fedha Pemba akichaguliwa Asya
Muhsini Omar aliyepata kura 25.

No comments:

Post a Comment