10 September 2012

BFT 'wakomaa' kufanya mashindano kama RT



Amina Athumani

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), litaendesha mashindano ya taifa ya mchezo huo kwa hali yoyote ile hata kama watakosa mdhamini.


Akizungumza kwa simu Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema mpaka jana zaidi ya mikoa 10 imethibitisha kushiriki mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Septemba 15, mwaka huu katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

Alisema bado hawajapata mdhamini wa kuweza kuyaendesha mashindano hayo ingawa mazungumzo bado yanaendelea baina yao na kampuni mbalimbali.

''Hali ya ukata katika shirikisho letu inajulikana lakini tumekuwa tukihaha kila kukicha kwa ajili ya kumpata mdhamini ambaye ataweza kuyaendesha mashindano haya ambayo ndiyo yaanayotoa taswira ya timu ya taifa ya Tanzania,''alisema Mashaga.

Alisema jumla ya sh. milioni 26 zinahitajika kuyaendesha mashindano hayo ambapo fedha hizo ni gharama ya malazi, chakula, vifaa vya mashindano kwa timu zote kutoka katika mikoa itakayoshiriki mashindano hayo.

Endapo mashindano hayo yatafanyika yatafanana na yale ya Riadha Taifa ambayo yalitarajiwa kumalizika jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambayo Chama cha Riadha Tanzania (RT) kilikosa mdhamini na kusababisha baadhi ya wanariadha wao kukimbia bila viatu huku wengine wakikwama mikoani.

No comments:

Post a Comment