10 September 2012
Mwanasheria amfungulia DC Korogwe kesi ya madai
Na Yusuph Mussa, Korogwe
HATIMAYE Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, mkoani Tanga, Bi. Najum Tekka, juzi ametimiza dhamira yake ya kumfungulia kesi Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Mrisho Gambo, kwa madai ya kumdharirisha na kudai fidia ya sh. milioni 96.
Akizungumza na gazeti hili jana, Bi. Tekka alisema kesi hiyo namba saba ya mwaka 2012, ameifungua katika Mahakama ya Wilaya ya Korogwe ili kulinda heshima yake kama mwanamke.
“Sijamshtaki Bw. Gambo, kama Mkuu wa Wilaya, nimefanya hivi bila kujali cheo changu wala chake, hata samansi ya kufika mahakamani Septemba 10 mwaka huu, nimeshampa ili kujibu madai yanayomkabili,” alisema Bi. Tekka.
Alisema ameamua kuongeza kiwango cha fidia kutoka milioni 90 hadi 96, kutokana na uzito wa jambo hilo juu ya udharirishaji aliofanyiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo.
Hivi karibuni, baadhi ya wafanyabiashara wa Soko la Manundu Mjini Korogwe, walidai kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya watendaji wa Serikali kushirikiana na wanasiasa ili kukwamisha jitihada mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Bw. Gambo.
Mwenyekiti wa Umoja wa wafanyabiashara sokoni hapo, Bw. Mussa Hussein, alisema hawakubaliani na njama zinazolenga kumdhoofisha ili ashindwe kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Wafanyabiashara hao walisema madai aliyotoa Bi. Tekka dhidi ya udharirishaji aliofanyiwa na Bw. Gambo hayana ukweli kwani hivyo kama Mkuu wa Wilaya atashtakiwa mahakamani, wapo tayari kumpa ushirikiano wakiamini madai hayo yamelenga kumchafua pamoja na kufifisha juhudi zake kiutendaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment