10 September 2012
Waliolala usingizi, taarifa za mapato na matumizi mnazihoji?
Na Godfrey Ismaely
KUNA fumbo kama si methali ambayo huwa inapambanua pande mbili za shilingi yaani ukimwamsha aliyelala na wewe utalala.
Wahenga wakaweka msamiati huu ili kuwanyamazisha wengi waliolala na mwisho wa siku usingizi unamfanya ajutie aliyelala huku aliyekuwa macho akiwa amefaidi mengi.
Hapo ndiyo panakuwa patamu kama aliyelala hakuweza kuzalisha japo kwa saa chache au kushiriki katika shughuli za kujenga taifa ndipo unazaliwa ugonjwa wa shida kama si malumbano ya aliyezalisha na aliyekuwa amelala.
Kanuni hiyo ilikuwa inaeda sambamba na sheria za upotoshaji kwa wakoloni kuwa 'Mjinga mwache alale, ukimwamsha utalala wewe' huku wakiendelea kujineemesha na mema ya Afrika wakati huo na hata sasa.
(
(Weka katuni picha hapa)
Wakati mwingine unaweza kuwaza ukagundua kuwa shida au matatizo ya Tanzania yanazalishwa na Watanzania wenyewe.
Shida ambazo wamekuwa wakizizalisha na zikianza kukomaa kama maembe kwenye mti zinaanza kudondoka kwa kishindo hivyo akipatikana mweneza propaganda za upotoshaji japo kidogo anawashibisha vilivyo na hoja zisisokuwa na mashiko.
Tukizungumzia shida au changamoto zinazowakabili Watanzania katika kaya, vitongoji, vijiji, mitaa, kata au tarafa utagundua kuwa asilimia kubwa zinachangiwa na wao wenyewe kutokana na kupuuzia baadhi ya mambo ya msingi.
MITAZAMO HASI
Uchunguzi wangu nilioufanya katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha baadhi ya wananchi kutoka mkoa wa Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Kisiwa cha Unguja, Arusha, Tanga na Manyara nimegundua kuwa Watanzania wana hulka ya kutoshiriki katika mikutano mbalimbali ya maendeleo.
Hali ambayo ni mbaya kuliko ugonjwa wa kifua kikuu maana unaweza kwenda hospitali daktari akakupangia taratibu za matibabu lakini ukishidwa kufika japo siku moja katika mikutano ya maendeleo ya vijiji au kata huwezi kupata tiba mahali popote maana umefukia haki yako.
Ni haki yako kwa sababu unajinyima fursa ya kuhoji taarifa za mapato na matumizi ya kijiji, mtaa au kata na namna ambavyo Serikali inatekeleza miradi ya maendeleo.
Kama miradi hiyo inatekelezwa ni kiasi gani cha fedha imetoa na ninyi wananchi mnapaswa kuchangia kiasi gani ili mwisho wa siku mliowapa dhamana ya kuisimamia muweze kuwahoji katika kikao kijacho zilivyotumika.
Mikutano ya wananchi na viongozi waliowapa dhamana hususan wajumbe, wenyeviti, watendaji katika ngazi za chini inawapa mwanya mzuri wa kuweza kuwatambua wabadhirifu wa fedha za miradi au wazoroteshaji katika miradi huska na ikiwezekana kupitisha maazimio ya nini kifanyike.
FAIDA YA MIKUTANO
Mikutano mbalimbali ya maendeleo au ya kujadili masuala ya msingi katika vijiji, mitaa au vitongoji ndiyo dira ya pekee katika kumuongoza mwananchi aliyeshiriki kuweza kuibua maovu, kero, pongezi au kutoa mtazamo chanya wa kujenga jumuiya yenu.
(Weka picha ya wananchi katika mkutano hapa)
VIONGOZI WACHOYO
Baadhi ya viongozi kwa sasa bila kujali kutoka chama tawala au vyama vya upinzani ambao mliwapa mamlaka ya kuwawakilisha katika ngazi za kutolea maamuzi wamekuwa wasahaulifu, wanapopata fursa huwa wanasahau shida mlizowaeleza awali lakini mna wajibu wa kuwakumbusha.
Unapozungumzia shida vivyo hivyo kundi la Watanzania kati ya milioni 40 nao wapo wanaolalama shida mno hivyo njia ya kuzitafutia ufumbuzi ni kukutana katika mikutano ya maendeleo ili kuzijadili na wakati huo huo unafanya kazi ipasavyo.
Kiongozi mchoyo ni vigumu kuwaamsha wananchi wake usingizini ili aweze kujineemesha na keki ya taifa mwenyewe, lakini ni vyema kuwaamsha wote na kuwashirikisha mbinu mbadala za kuondoka katika hali waliyonayo.
Lawama za ufisadi, wizi, mmomonyoko wa maadili nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na watu wanaopenda wengine walale ili wao waweze kujineemesha, hivyo ndiyo ilivyo kwa viongozi wa Tanzania.
Hivyo katika kuwaamsha Watanzania lazima washirikishwe katika mbinu za kujikomboa na hali ngumu ili kupunguza lawama na malalamiko yanayoongeza mgawanyiko na makundi yasiyokuwa ya msingi.
HALMASHAURI ZINAVYOWAKWAMISHA
Halmashauri zinaposhindwa kutumia fedha zilizotengwa kwa miradi ya maendeleo kwa wakati uliopangwa katika serikali za mitaa huchangia huduma na manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii yanacheleweshwa.
Pia huchangia gharama zinaendelea kupanda na kwa vile mfumuko wa bei unashusha thamani ya fedha iliyotengwa katika bajeti, ni huduma chache tu ndizo zinazoweza kupatikana ikilinganishwa na zile zilizopangwa awali.
Hali hiyo huchangia matatizo lukuki na kama wananchi walikuwa wamelala bila kuhoji taarifa za mapato na matumizi, mambo huwa mabaya baada ya kuonekana halmashauri nyingi hazitumii ruzuku za maendeleo kikamilifu na kwa wakati uliopangwa ili kuwafikishia wananchi huduma muhimu.
UVIVU UNAVYOAKISI AIBU
Mamlaka za serikali za mitaa zina wajibu wa kukusanya mapato katika sehemu zao yaani kutoka kwa wananchi ili kuongezea katika fedha zinazopokea kutoka Serikali Kuu na zimeruhusiwa kutumia mawakala kukusanya mapato hayo.
Njia pekee ya kufanikisha hayo ni kupitia ushirikishwaji kutoka kwa wananchi, serikali na mawakala ili waweze kutambua muda wa makusanyo, kiasi kilichopatikana na kilienda kufanya nini.
Wakati mawakala wanapotumiwa, mamlaka za serikali za mitaa zina jukumu la
kuwasimamia ili kuhakikisha wanafanya marejesho sahihi ya mapato kwa wakati ili mwisho wa siku waweze kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa wanachi.
Huwa unafika katika mikutano ya maendeleo ya vijiji, mitaa au vitongoji na kama huwa unafanya hivyo kwa mwezi au baada ya miezi mitatu huwa unahoji taarifa za mapato na matumizi? Jaribu kufanya hivyo uweze kuamsha uwajibikaji.
Viongozi uliowapa dhamana ya kukuwakilisha wanatumia vema nafasi zao kuwasomea vipaumbele vya maendeleo au huwa wanaitisha mikutano mara kwa mara katika kijiji au mtaa? Ushauri au maoni; 0719-254464 barua pepe; ismaelygodfrey@gmail.com.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment