10 September 2012

Mwanafunzi IFM mbaroni kwa mauaji



Na Faida Muyomba,
Geita

JESHI la Polisi mkoani Geita, linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es salaam, Bw. Yohana Bundala (22), kwa tuhuma za kumnyonga na kumuua mlinzi wa jadi (sungusungu).


Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Septemba 4 mwaka huu, saa tano usiku katika Kitongoji cha Ludete, Kata ya Katoro, wilayani Geita.

Alimtaja mlinzi huyo kuwa ni Yohana Tabu (28) ambapo chanzo cha mauaji hayo ni mtuhumiwa kumshambulia Bw. Bado Keya (27), ambaye alikwenda Ofisi za Sungusungu kuomba msaada.

“Baada ya taarifa hizo kufikishwa Ofisi ya Sungusungu, marehemu aliongozana na mwenzake ili kwenda kumkamata mtuhumiwa ambaye baada ya kumchukua, wakiwa njiani kwenda ofisini, mtuhumiwa alimkaba marehemu shingoni na kumuua.

“Mtuhumiwa alitoroka lakini baadae alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi kilichopo eneo la Katoro ambako baada ya kumpekua, walimkuta na kitambulisho cha chuo na atafikishwa mahakamani muda wowote,” alisema Kamanda Paulo.

No comments:

Post a Comment