17 September 2012
Mgeja: Wana CCM acheni malumbano
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Shinyanga, wametakiwa kuacha malumbano yasiyo na tija katika kipindi hiki ambacho chama hicho kinafanya chaguzi mbalimbali.
Hali hiyo inaweza kukiathiri chama hicho badala yake wanachama wawe na mshikamano ambao utasaidia kuijenga CCM.
Ushauri huo umetolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM, mkoani hapa, Bw. Khamis Mgeja wakati akifungua Kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa ambacho kilikuwa kikijadili majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa.
Akizungumzia mchakato wa uchaguzi unaoendelea, Bw. Mgeja alisema wana CCM wanapaswa kuwa makini kwa kuendesha kampeni za kistaarabu bila kutunishiana misuli.
“Chaguzi zinazoendelea ndani ya CCM, zisiwagawe wanachama kwani hali hii inaweza kukiathiri chama katika Uchaguzi Mkuu 2015, nguvu zinazotumika kurushiana makombora ni vyema zikatumika kuwatumikia Watanzania.
“Wananchi wanakabiliwa na kero mbalimbali, ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira na tatizo la rushwa hivyo suala la ushirikiano na mshikamano katika kipindi hiki cha uchaguzi ndani ya chama ya CCM ni muhimu sana kuliko wakati wowote,” alisema.
Aliongeza kuwa, hakuna haja ya wana CCM kutunishiana misuli wanapowania nafasi za uongozi kwani wote ni kitu kimoja hivyo uchaguzi usiwe kigezo cha kuwagawa na kuchafuana.
Alisema yeye binafsi anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kumaliza kipindi chake cha uongozi bila tuhuma yoyote ambayo ingesababisha afikishwe katika vikao vya maadili au kupewa onyo.
Aliwaomba wana CCM kujenga tabia ya kusamehe wanapokosana kwa mambo madogo kwani palipo na watu wengi, lazima tofauti ijitokeze miongoni mwao na hakuna binadamu aliyekamilika.
Bw. Mgeja aliwahadharisha baadhi ya viongozi wa CCM ambao wameanza kuingilia chaguzi za jumuiya katika chama hicho, waache mara moja kwani kitendo hicho ni sawa na kuwapokonya wagombea uhuru na haki yao kikatiba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment