17 September 2012

NI MAJONZI MAKUBWA Bwana harudi afariki ghafla *Mauti yamkuta usiku familia ikiwa kwenye mkesha *Harusi ilikuwa ifungwe jana, mazishi kufanyika leo


Na Stella Aron

KATIKA hali isiyo ya kawaida, harusi iliyokuwa ifungwe jana mchana, imeingia dosari baada ya bwana harusi mtarajiwa, Rashid Hamad, kufariki ghafla juzi usiku wakati familia yake ikiwa katika mkesha wa kusheherekea ndoa hiyo.


Tukio hilo la kusikitisha limeitokea familia ya Mzee Hamad, mkazi wa Ukonga Mzambarauni, Dar es Salaam na kusababisha nderemo na vifijo vya harusi hiyo kugeuka majonzi baada ya familia, ndugu na jamaa kupata taarifa za msiba huo.

Kifo hicho kilitokea saa nane usiku wakati ndugu na jamaa wa marehemu, wakiendelea kuburudika na muziki wa taarabu.

Akizungumza na gazeti hili jana nyumbani kwa wazazi wa marehemu eneo la Mzambarauni Shule, Bw. Ally Khatibu, ambaye ni baba mkubwa wa marehemu, alisema kifo hicho kimeishtua na kuisikitisha familia yao bila kujua nini cha kufanya.

Alisema kifo cha mtoto wao kimetokea ghafla wakati familia hiyo ikiendelea na utaratibu wa kusheherekea harusi yake.

“Mtoto wetu alikuwa kondatka na alitarajia kumuoa binti anayeitwa Kuruthumu, taratibu zote za ndoa siku ya leo (jana), zilikamilika na familia ilikuwa katika mkesha wa shughuli yake.

“Siku nzima ya jana (juzi), tumeshinda na marehemu na hakulalamika kuumwa mahali popote, usiku alikuwa akicheza muziki na vijana wenzake pamoja na wafanyakazi wenzie, kwa kweli nashindwa hata kuelezea msiba huu,” alisema Bw. Khatibu.

Akizungumzia mazingira ya kifo hicho, alisema marehemu alilala mapema lakini rafiki pamoja na ndugu zake walimuomba aamke na kutoka nje ili waweze kusheherekea pamoja.

Alisema kutokana na pilika nyingi za maandalizi ya harusi yake, marehemu alikuwa amechafuka mwili mzima hivyo aliamua kwenda kuoga na baada ya kuingia ndani, ghafla alipiga mayowe ya kuomba msaada akidai anakufa.

“Kutokana na mayowe hayo, ndugu waliokuwepo waliingia ndani  ndipo tulipokuta kijana wetu amekata kauli ghafla na kudondoka chini hivyo walimkimbiza Zahanati ya MICO iliyopo, Mzambarauni,” alisema Bw. Khatibu.

Aliongeza kuwa, madaktari wa zahanati hiyo walishauri marehemu apelekwe Hospitali ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kilichopo Ukonga ambao nao walishauri akimbizwe Hospitali ya Wilaya Amana, wakidai hali ya mgonjwa si nzuri.

Alisema baada ya kufikishwa Amana, wauguzi walimuingiza wodini lakini kwa bahati mbaya tayari alikuwa amefariki dunia.

“Kwa kweli hatukuamini tulichoambiwa, hadi sasa hatuelewi kilichomsibu kijana wetu kama ni shoti ya umeme au kuna jambo lingine,” alisema.

Bw. Khatibu alisema tayari wamekaa kikao cha familia na kuamua waache kuchunguza zaidi chanzo cha kifo hicho bali wamemuachia Mungu na wamekubaliana kumzika leo katika Makaburi yaliyopo Kimanzichana Mkuranga.

Hata hivyo, familia hiyo imefungua jarada la taarifa ya kifo hicho Kituo cha Polisi Stakishari na kupewa RB namba STK/RB/16096/2012.

3 comments:

  1. Inasikitisha sana!Isipokuwa siku zote tunaambiwa kesheni mkiomba hamjui siku wala saa.

    ReplyDelete
  2. INNALILLAHI WAINNA ILAIHI RAJIUNI. KINACHOHITAJIKA KWA FAMILIA NI SUBRA NA UVUMILIVU. NA HAINA HAJA YA KUFANYA UCHUNGUZI KWANI KILA NAFSI ITAONJA UMAUTI HIVYO CHOCHOTE KITACHOBAINIKA ITAKUWA NI SABABU TU KATIKA SABABU ZA KIFO CHAKE. CHA MSINGI TULIO HAI IWE FUNDISHO KWETU TUACHE MAASI KWANI HATUJUI NI LINI NA SAA NGAPI TUTAKUFA.

    ReplyDelete