07 September 2012

'IGP watazame upya makamanda wako'


Na Stella Aron

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, kuwatazama upya baadhi ya makamanda wake ambao wanafanya kazi zao kinyume cha sheria ili kudumisha amani inayotaka kupotezwa na polisi.

Naibu Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, Bw. Abdul Kambaya, aliyasema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana baada ya Mbunge wa Kilwa Kusini kwa tiketi ya CUF, Bw. Selemani Bungara, kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kufanya vurugu kwenye Kituo cha Polisi wilayani humo.

Bw. Kambaya alisema CUF inalaani kitendo cha Jeshi la Polisi wilayani humo kumkamata mbunge wao na kumfungulia mashtaka kwa madai ya uongo.

“Baadhi ya vitendo vinavyofanywa na polisi ni sawa na sikio la kufa lisilo kubali dawa hivyo IGP Mwema anapaswa kuangalia upya makamanda wake,” alisema Bw. Kambaya.

Alisema IPG Mwema anapaswa kuwa na makamanda waadilifu wasiojiingiza katika shughuli za kisiasa ili kudumisha amani ambayo inaonekana kupotezwa kwa makusudi na baadhi ya watendaji wake.

“Kitendo cha kukamatwa mbunge wetu kwa madai ya kugushi ni kuamsha hasira za wanachama wetu inchi nzima, kwa muda mrefu CUF tumekuwa tukihimiza uvumili wa kisiasa na umuhimu wa kutunza amani dhana ambayo inatumiwa vibaya na polisi,” alisema.

Alidai Agosti mwaka huu, Katibu wa CUF wilayani humo alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa rushwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kilwa.

“CUF tunalitaka Jeshi la Polisi kutafakari na kujali masilahi ya Taifa badala ya kufanya kazi kinyume na utaratibu ili Watanzania wasikose imani na jeshi lao,” alisema.

Bw. Kambaya aliongeza kuwa, chama hicho kinalitaka jeshi hilo kutafakari kwa kina kuhusu mwenendo wake wa kuhudumia Watanzania na kama tabia hiyo itaendelea, wataandaa maandamano makubwa wilayani humo ili kufikisha ujumbe huo.


No comments:

Post a Comment