17 September 2012

Familia 11 zachomewa makazi, polisi walaumiwa



Na Timothy Itembe, Rorya

FAMILIA 11 zilizopo Kijiji cha Nyambogo, Kata ya Kitembe, Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, hazina mahali pa kulala baada ya makazi yao kuchomwa moto na wananchi wenye hasira.


Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Kaimu Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Gereshoni Nyakore, alisema tukio hilo limetokea juzi saa saba mchana.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni baada ya vijana wa familia ya Agaka Otieno, kumvamia Bw. Ochieng'i Oswaga na kuanza kumshambulia kwa kipigo wakidai aliwataja kwenye kikao cha wazee wa mila na kudai familia hiyo ni wachawi.

“'Baada ya shambulio hilo, Bw. Ochieng'i alikimbilia Ofisi ya Serikali ya kijiji huku akipiga yowe, wananchi walikuja na kushindwa kujizuia kutokana natukio hilo.

“Wananchi waliamua kwenye kuchoma moto miji yote ya watu waliotajwa kuhusika na mambo ya uchawi ambayo ni kaya zake zinahusisha familia ya Agaka Otieno, Agose Akwaa, Otieno Oduli, Okechi Jasem, Otieno Nyang'au, Okole Matoyo na Otieno Kwai.

Katika tukio hilo, Jeshi la Polisi wilayani humo lilitupiwa lawama kwa kushindwa kudhibiti vurugu hizo mbali ya kuwa na taarifa.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walisema mikutano yote iliyoitishwa kijijini hapo kujadili mambo ya uchawi, iliibua hasira za wananchi ambao tangu awali walionesha dalili za kuchoma moto nyumba za familia zilizotajwa kuhusika na uchawi.

“Hasira za wannchi zilikuwa zikitulizwa na Diwani wakata hii hivyo Jeshi la Polisi lilipaswa kujipanga na kuimarisha ulinzi kijijini ili kuzuia janga ambalo limetokea kwani polisi walishiriki mikutano yote iliyofanyika ili kukusanya maoni ya wananchi.

“Jambo la kusikitisha watuhumiwa waliojajwa walikamatwa na baadae kuachiwa huru hivyo walirudi kwa wannchi na kufanya fujo ambazo ndio zilisababisha uchomaji wa nyumba,” alisema.

Mbunge wa jimbo hilo, Bw. Lameck Airo, aliahidi kwenda kufanya mahubiri katika eneo hilo kupitia Kanisa la Wasabato.

“Nitahakikisha Wasabato wanafanya mahubiri kijijini hapo ili kuokoa maisha ya watu wanaouliwa bila sababu, naamini Mungu atafanya maajabu yake kwa kutoa uchawi ili tabia hiyo ikome na wananchi waokoke,” alisema alisema Bw. Airo.


No comments:

Post a Comment