17 September 2012

CCM Sengerema waandamana kushinikiza viongozi kujiuzulu


Na Faida Muyomba, Sengerema  

BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwemo viongozi wa mashina na matawi katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza, mwishoni mwa wiki walifanya maandamano ya amani kushinikiza viongozi wa chama hicho wilayani humo kujiuzulu.


Wanachama hao wanadai kuwa, viongozi wa CCM wilayani humo wameshindwa kusimamia rasilimali ukiwemo ujenzi wa ofisi ya chama hicho ya Wilaya.

Waandamanaji walikusanyika katika Ofisi za CCM wilayani humo ambako kuna ujenzi wa jengo la ofisi ya chama hicho ambalo limeshindwa kukamilika kutokana na usimamizi mbovu.

Baada ya kufika eneo hilo, baadhi ya waandamanaji wakiwa na mabango mbalimbali na mkataba wa ujenzi wa jengo hilo, waliazimia kufikisha kilio chao kwa uongozi wa CCM Mkoa.

Maandamano hayo yalipokelewa na aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi mkoani Mwanza, Bw. Kibisa Muyoba, ambapo aliyekuwa Katibu CCM, tawi la Busisi, Bw. John Dickson, aliwasilisha taarifa ya waandamanaji na kusema hawako tayari kufumbia macho vitendo viovu ndani ya chama hicho.


Kwa mujibu wa mkataba na ujenzi huo, ujenzi wa ofisi hiyo ulipaswa kukamilika na kukabidhiwa Aprili 24,2009 na baada ya muda huo kupita alitakiwa kulipa fidia ya sh. 50,000 kila siku.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM, wilayani humo Bi. Magreth Ndwete, alikiri kuwepo malalamiko ya ujenzi huo kutokamilika katika muda uliopangwa, kutokana na uzembe wa baadhi ya viongozi na kukanusha kuwepo ubadhirifu.

Alisema Agosti 31 mwaka huu, yeye na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, walimpa mkandarasi siku 45, kukamilisha ujenzi huo vingenevyo atachukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment