17 September 2012

Wakamatwa na fedha bandia euro mil. 10


Na Willbroad Mathias

JESHI la Polisi Kikosi cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kinawashikilia Watanzania wawili waishio nchini Afrika Kusini baada ya kukamatwa wakiwa na euro bandia zenye thamani inayokadiliwa kufikia sh. milioni 10.

Vyanzo vyetu vya habari vimedai kuwa, watuhumiwa hao ni mwanamke na mwanaume ambao walikamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa, kabla ya kukamatwa ulitokea mvutano kati ya mtuhumiwa mwanamke na mwenzake ambaye waliambatana katika uwanja huo wakati mtuhumiwa mwanaume akiwa ndani.

Hali hiyo iliwafanya polisi kuingiwa na shaka hivyo walianza kufuatilia kile kinachobishaniwa.

“Kabla ya kuwakamata watuhumiwa, ulitokea mvutano wakati huo mtuhumiwa wa kiume alikuwa katika chumba cha mapumziko tayari kwa safri ya kwenda nchini Afrika Kusini.

“Baada ya polisi kubaini chanzo cha mabishano hayo, waliamua kumsaka mtuhumiwa wa kiume na kumfanyia upekuzi upya ndipo alipokutwa na euro bandia,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa, mbali ya kukamatwa na euro hizo mtuhumiwa huyo pia alikutwa na fedha nyingine za Kitanzania zinazokaribia kufikia sh. milioni tatu pamoja na hati mbili za kusafiria moja ya Tanzania na nyingine Afrika Kusini.

Akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Kamishna Mkuu wa Kikosi hicho, Kamanda Ulrich Matei, alisema walikamatwa saa tisa alasiri na kuwataja majina yao kuwa ni Bw. Omary Salum na Bi. Khadja Yusuf, ambao wanaishi nchini Afrika Kusini.

Alisema kwa mujibu wa maelezo ya Bw. Salum, alikuja ili kununua dhahabu na kopa mjini Songea, mkoani Ruvuma, lakini baada ya kufika mkoani humo alikuta biashara ni ngumu akaamua kuondoka.

Aliongeza kuwa, Bw. Salum baada ya kufika Dar es Salaam, alikuwa apokelewe na Bi. Yusuf, ambaye kwa sasa yupo Tanzania lakini anaishi nchini humo.

Hata hivyo, Kamishna Matei alisema baada ya kuhojiwa, Bw. Salum alidai fedha hizo alibadilishana na raia mmoja wa China ambapo yeye alimpatia randi 70,000 na kupewa kiasi hicho cha fedha.

Akizungumzia mazingira yaliyosabisha kukamatwa kake, Kamanda Matei alisema siku ya tukio Bw. Salum alikuwa akutane na Bi. Yusuf, uwanjani hapo.

“Bw. Salum alipofika uwanja wa ndege, mwenyeji wake Bi. Yusuf alikuwa amechelewa, muda wote walikuwa wakiwasiliana kwa simu ya ofisa wetu mmoja kwani mtuhumiwa hakuwa na laini ya simu za Tanzania,” alisema Kamanda Matei.

Alisema baada ya muda mfupi, Bi. Yusuf aliwasiri uwanjani hapo akiwa na mwanamke mwingine aliyemtaja kwa jina la Bi. Zamzam Shaban.

Bi. Shaban aliuliza alipo Bw. Salum na baada ya kuambiwa tayari ameingia ndani, alianza kulalama na kudai mtuhumiwa alikuwa mpenzi wake na walikubaliana ampe pesa badala yake amemtoroka hivyo aliamua kutoa siri ya mtuhumiwa kufanya biashara ya kuuza noti bandia.

Alisema hivi sasa wanamshikilia Bi. Yusuf kwa sababu baada ya Bi. Shaban kutoa siri hiyo, alituma ujumbe mfupi (sms), kumjulisha Bw. Salum kuwa atafute njia ya kujinusuru.

Ujumbe huo ulitumwa katika simu ya ofisa huyo baada ya Bi. Yusuf kudhani kuwa, simu hiyo ilikuwa ya mtuhumiwa ambapo kazi ya kumsaka Bw. Salum, ilianza na kukamatwa.


No comments:

Post a Comment