16 August 2012
Toto la Simba laiua Azam *Sasa kukutana na Mtibwa fainali
Na Speciroza Joseph
MABINGWA Tanzania Bara Simba, ambao jana walichezesha timu B wamefanikiwa kutinga fainali ya michuano Kombe la Super 8 baada ya kuizaba Azam FC mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo Simba B, ambayo imewalipia kisasi kaka zao ambao walifungwa mabao 3-1 na Azam katika michuano ya Kombe ka Kagame, itamenyana na Mtibwa Sugar katika fainali itakayochezwa Jumamosi.
Simba ndiyo ilianza kupata bao dakika ya pili lililofungwa na Rashid Ismail kwa shuti kali, lililokwenda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa wa Azam Jackson Wandwi, asijue la kufanya.
Dakika ya 18 Kipre Tchetche, alipata nafasi nzuri akiwa na kipa wa Simba Abuu Juma, ambaye aliokoa kwa ustadi mkubwa.
Tchetche alipata nafasi nyingine nzuri dakika ya 22, hata hivyo shuti lake likapaa nje lango la Simba.
Katika kipindi hicho kikosi cha Simba B, kilionesha kandanda safi na kuwapeleka puta Azam na kuwafanya mashabiki wa mabingwa hao wa Tanzania Bara, kulipuka kwa furaha kila wachezaji wake walipogusa mpira.
Kipindi cha pili Azam ilifanya mabadiliko kwa kumtoa, Jabir Aziz na nafasi yake kuchukuliwa na Himid Mao.
Mabadiliko hayo hayakuisaidia kitu Azam kwani dakika ya 56, Simba ilipachika bao la pili kwa penalti iliyotumbukizwa wavuni na Edward Christopher.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya beki wa Azam, Said Morad kumchezea rafu katika eneo la hatari Christopher aliyekuwa akielekea kufunga.
Kocha wa Azam, Kally Ongara baada ya kuona mambo yanazidi unga aliwatoa Tchetche, Sunday Frank na Gaudence Mwaikimba wakaingia Mcha Khamis, Kelvin Friday na Zahoro Pazi.
Simba iliwatoa Frank Sekule, Omari Salum na Christopher ambao waliumia wakaingia, Ibrahim Hajibu, Ramadhan Mzee na William Lucian.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Azam ambayo dakika ya 73, ilipata bao kupitia kwa Pazi, aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Abdi Kassim 'Babi'.
Katika mechi ya nusu fainali ya kwanza, iliyopigwa saa 8 mchana katika uwanja huo, Mtibwa Sugar ilifanikiwa kupenya hatua ya fainali baada ya kuikandika Jamhuri ya Pemba, mabao 5-1.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment