08 December 2010

Wenje achangiwa samani za ofisi

*Ni baada ya Masha kudaiwa kuzihamisha
*Zitto apuunza madai mgawanyiko Chadema


Na Wilhelm Mulinda, Mwanza

WANANCHI wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza juzi walichanga sh 179, 690 kwa ajili ya kununua samani za Ofisi ya Mbunge wa
Jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Ezekia Wenje.Fedha hizo zilichangwa wakati mbunge huyo alipokuwa akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Sahara jijini hapa kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua.

Wananchi hao waliamua kuchanga fedha hizo baada ya mbunge huyo kueleza kuwa ofisi yake haina meza wala kiti na kwamba analazimika kuwahudumia wananchi akiwa amesimama kutokana na samani ambazo zikuwa katika ofisi hiyo kuchukuliwa na Mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Bw. Lawrence Masha kwa madai kuwa alinunua samani hizo kwa fedha zake.

Siku chache baada ya Bw. Masha kuachia madaraka hayo, iliyokuwa ofisi yake ilikuwa haina samani muhimu, ikiwamo picha ya Rais Jakaya Kikwete, simu ya mezani ilikatwa waya na kichwa chake kubebwa; vitasa, zulia, mafaili yenye nyaraka za maendeleo ya jimbo na mapazia.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Wenje alikaririwa akisema: Niliwabana viongozi ngazi ya wilaya na mkoa wanieleze vimeenda wapi hivi vitu… niliambiwa eti vilinunuliwa na mtu binafsi na havikuwa vya serikali.Akihutubia mkutano huo juzi Bw. Wenje alisema kuwa Bw. Masha hakuwa na sababu ya kuchukua samani hizo kwa vile serikali kila mwaka ilikuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuendesha ofisi hiyo na kuhoji kwamba kama alinunua kwa fedha zake, zile za serikali zilienda wapi kwa kipindi cha miaka mitano.

Akiwashukuru wananchi, Bw. Wenje alisema kuwa yeye amekuwa mbunge kwa sababu wananchi walikubali kupigwa mabomu na hata kupoteza maisha yao siku ya kutangaza matokeo, na si kwa sababu alipigiwa kura nyingi au nchi ni ya demokrasia.

Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza siku ya kuwachagua Meya na Naibu Meya wa Jiji hilo ili washangilie ushindi, kwa vile chama chao kina wajumbe wengi wa kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo ambao wanakihakikishia ushindi wa kutwaa viti hivyo na kuongoza halmashauri hiyo.

"Sisi tuna wajumbe 17 ukiweka na diwani mmoja wa Chama cha Civic United Front (CUF) tunakuwa jumla 18 wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kina wajumbe 13 pekee, hivyo hatuna sababu ya kushindwa kupata kiti cha umeya na naibu meya," alisema Bw. Wenje.

Bw. Wenje alisema kuwa endapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itahitaji kuwaondoa wamachinga katika maeneo wanayofanyia biashara, inatakiwa kufanya nao mazungumzo badala ya kuwaondoa kwa nguvu, hali ambayo inaweza kusababisha kero kwa wafanyabiashara hao na wananchi wengine kwa ujumla.Alisema kuwa yeye amechaguliwa na maskini, hivyo ni lazima asimame mstari wa mbele kuwatetea wanyonge ambao ndio wapiga kura wake, ili wafanye shughuli zao za kujiletea maendeleo pamoja na familia zao bila usumbufu wowote.

Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu Rehema Mohamed anaripoti kuwa chama hicho kimesema kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya chama hicho unaosababisha wanachama wake kutambuana kwa uvaaji wa sare za chama hicho kuwa wafuasi wa kiongozi fulani.

Akizungumza na gazeti hili, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Bw. Erasto Tumbo alisema hoja hizo hazina mashiko kwa kuwa suala la mavazi linatokana na mapendekezo ya mtu mwenyewe.Bw. Tumbo alisema mtu anayeongozwa kwa mavazi ni yule aliyefilisika kifikra na anahitaji msaada kuondokana na hilo.

"Hoja hiyo haina mashiko yoyote, uvaaji wa fomu ni kutokana na mtu anavyopenda kuvaa, binadamu mwenye akili timamu hawezi kuongoza fikira zake kimavazi, mimi nina sare zote za mikono mirefu na mifupi, je, ni mfuasi wa nani kati ya hao?, alihoji Bw. Tumbo

Akizungumzia madai ya kuwepo kwa udini ndani ya chama hicho, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa anayepaswa kulisemea ni Bw. Zitto aliyedaiwa kulitamka.Kwamujibu wa taarifa iliyochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari jana ilibainishwa kuwa kuna mvutano wa uongozi ndani ya CHADEMA na kusababisha mgawanyiko wa wanachama kulingana na uvaaji wa sare za chama hicho.

Ilibainishwa kuwa wanachama wanaovaa sare za mikono mifupi ni wafuasi wa Naibu Katibu Mkuu, Bw. Zitto Kabwe na wale wanaovaa kombati za mikono mifupi ni wafuasi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe.

Lakini pia madai hayo yamekanushwa na Bw. Kabwe kwenye mtandao wake wa Wordpress.com kuwa habari hizo ni za kutunga zenye lengo la kugawa uongozi wa CHADEMA na kuleta mgogoro."Kumekuwa na habari kwenye magazeti kitambo sasa zenye kuonyesha mgogoro ndani ya CHADEMA. Napenda kuwajulisha marafiki zangu kuwa hakuna mgogoro wowote. Sihami wala sifukuzwi CHADEMA," alisema Bw. Kabwe.

Aliongeza kuwa, "Tuna kazi moja tu, nayo ni kuimarisha chama kuelekea 2015 wakati tukipigania mabadiliko ya katiba. Tusiyumbishwe!"

13 comments:

  1. sumu imeshaingia katik blood system ya chadema! inatambaa taratibu na mwishowe ni kuua kabisa hicho chama kama hamna habari! Tafuteni anti-poison mapema, anzeni na maziwa kuiua nguvu

    ReplyDelete
  2. mbona nyinyi Chadema mnaupenda sana huu UDUNI UDINI, tumekuwa tukiwasikia sana wanachama na wafuasi wa chadema wakiuuzungumza sana udini. jee mmeshaiandaa nchi na vita hii ya udini mmejiamini kiasi gani kuwa mtashinda kwa hilo.?

    ReplyDelete
  3. wewe bwana nani hii hapo juu,acha fikra potofu.My be anaye fikiria udini ni wewe na mshauri wako KDDDK.

    ReplyDelete
  4. Anonymous hapo juu, UDINI ni propaganda za CCM ambazo zilichochewa zaidi sana na mgombea wao Jakaya wakati akijinadi kupata kura. Dhana hiyo ilishereheshwa na magazeti ya Rostam Aziz. Au unajifanya hufahamu hilo? Hitimisho ni hili lililotolewa na Sheikh Mkuu kuwa serikali imeridhia kuanzishwa kwa mahakama ya Kadhi. Hili nalo "NENO"! Hakika ya hili ilitolewa na Gharib Billal wakati wa sikukuu ya Kiislam hivi karibuni. Upo hapo? Wakristo sijui mahakama yao itakuwa ni ipi!

    ReplyDelete
  5. Ni kweli, mchangia wa hoja ya kwanza na ya pili ni watu wenye fikra potofu za CCM. nani asiyejua kuna baadhi ya misikiti ilitumika wazi wazi kuhusu kumchagua rias m-islam wakati wa kampeni za chama cha mapinduzi? Naunga na mchango wa mtu wa mwisho kuwa uduni ni sera zilizotumika na ccm kuwadanganya umma kuwa vyama vya upinzani vinatumia udini na vita!! NASEMA WANATAKA KUCHAFUA NCHI NI CCM!!!!!!

    ReplyDelete
  6. Machinga sasa wako katika kila maeneo ya jiji la Mwanza na kusababisha kero wakiacha yale maeneo waliyotengewa maalum.

    Kuwaondoa kwa kuwabembeleleza kunawezekana tu kama Mh.Wenje atakuwa mstari wa mbele kukaa nao na kuwaambia kuwa msongamano wao katika jiji unapoteza hadhi ya jiji la Mwanza.

    ReplyDelete
  7. Jamani huyu Mbunge achangaiwe samani za ofisi yake na wananchi kwani pesa zake za kutoka bungeni kafanyia nini au kapeleka wapi? Si kila mbunge ana fungu lake la mambo ya ofisi, na pia anapewa posho kubwa tu karibu hiyo waliyomchangia kwa siku?

    Mambo mengine ni aibu hata kuyasema hadharani kweli Mbunge mzima uchangiwe laki moja na wananchi masikini kisha unapokea badala ya wewe kuwachangia kwenye shughuli zao za maendeleo? Kujiendekeza huku kubaya au ndio madeni ya kampeni bado hayajaisha?

    ReplyDelete
  8. Mbunge mzima analilia vya wenzie, yeye kama Mbunge si alijiamisha kwa wananchikwamba anao uwezo wa kila kitu, anashindwa nini kununua vtya kwake hadi achangiwe? What is Laki moja na uchafu? Anatia aibu, mtu mzima analilia samani za ofisi, buy your own property man!!! yeye wa CCM kaenda na vya kwake nawewe njoo na vyako, aache ushamba.

    ReplyDelete
  9. mnashangaa mbuge kuchangiwa samani?mbona nyerere alichangiwa elfu 6!akidai uhuru, acheni firkira mfu mbona hamulizi imekuwaje masha kuondoka nazo?tafadhali hio 179,000 ni alama nzuri ya sauti ya umma na bado mpaka kitaeleweka, wenje hongera sana

    ReplyDelete
  10. JE HUU NDIO MWANZO WA MWISHO KWA MWANZA NA JIJI LAKE? Historia hujirudia: Mwaka 1990, wanaMwanza tulishabikia saana, tena sana harakati na kampeni za Mh. mmoja aliyekuja na lugha, wajihi na hata vuguvugu kama la WENJE. Jimbo ambalo mpaka wakati huo liling'ara kwa barabara za lami na taswira nzuri za bustani, ghafla likasimama shime kudai mabadiliko hata hakuna ajuaye ya kwenda wapi!!

    Leo hii, miaka 20 kamili, Mwanza akiwa inang'ara, taswira nzuri na mandhari ya kupendeza kama Jiji, limesimama shime kudai mabadiliko - ya kwenda wapi, sina hakika kama kuna ajuaye!!

    Kama ilivyokuwa 1990 - Ofisi ya Mbunge iliyojaa Samani, ilikosa mkazi baada ya miezi 6 tu. Pakaota utando wa buibui! "Mkombozi" yule akaingia, akatoka... kumbe uongozi si lelemama, na kusimamia raslimali nyingi za kuendesha jiji kama Mwanza sio mbina inayochezwa na wana Mwanza hapo hapo Mwanza, bali ni kazi ya ziada kuvuta raslimali toka pande zote, hususan HAZINA KUU. Ghafla milango ya raslimali iliyokuwa wazi kwa makusudi, taratibu ikaanza kufunga, sio kwa ajili ya kunyimwa, bali kukosa mbinu na uzoefu wa kuzifuatilia, na pale zinapokuja, kuzisimamia ipasavyo raslimali hizo. Matokeo? Miaka 5 - 10 baada ya hapo Jiji la Mwanza likarudi kuwa kama mji mwingine wowote mdogo, vumbi, rabsha, kila mahala soko, kila kichochoro kibanda cha biashara... ilikuwa mwanzo wa mwisho, ukafika mwaisho wake.

    BASI NA LEO - TUTAFAKARI, JEE HAYA TUNAYOYAONA NDIO YALE YALE YA MIAKA 20 ILIYOPITA? MUUJIZA GANI TUNAUTARAJIA KUTOKA MTEULE WETU?? YETU NI MACHO!

    ReplyDelete
  11. Ifike mahala watanzania tuanze kuamka kuchangiwa ni utamaduni wetu halijalishi umaskini au la cha msingi ni kujua mbunge aliyepita kasma ya ofisi alikuwa anapeleka wapi? hiyo ni dalili tosha kuonyesha kuwa wabunge wetu sio waaminifu wajirekebishe ili kusaidiana na wananchi kuondoa umaskini

    ReplyDelete
  12. Mbunge akisha chaguliwa anafanya kazi kwa ajili ya watu wote katika jimbo lake. Siyo tu kwa ajili ya wale waliomchagua.Usiwagawe wananchi wako katika makundi makundi. Utasababisha chuki.

    ReplyDelete
  13. kama ninyi chadema mmechagua njia hii na mnaiamini kuwa ni njia sahihi fine!sisi wafuasi wenu nasi tutaamua njia.

    ReplyDelete