16 August 2012

Yanga, Coastal kisasi J'tatu



Na Mwandishi Wetu

TIMU za Yanga na Coastal Union ya Tanga, zinatarajia kuumana katika mechi ya kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara ambayo itapigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumatatu ya wiki ijayo.

Mechi hiyo inatarajia ya kuwa na visasi, kwani mara ya mwisho timu hizo zilipokutana kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, Yanga ilinyang'anywa pointi tatu baada ya kumchezesha Nadir Haroub 'Canavaro', aliyekuwa na kadi tatu nyekundu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mratibu wa mechi hiyo, Juma Athuman alisema lengo la pambano hilo ni kuwatambulisha wachezaji wapya timu hizo, ambao wamesajili kwa ajili ya msimu mpya wa ligi.

"Tunatarajia mechi itakuwa nzuri kwa kuwa Yanga ambayo imesajili wachezaji wakali, itataka kuonesha kwamba ilinyang'anywa pointi katika ligi kimakosa huku Coastal nayo ikijagamba kwamba wako fiti," alisema Athuman.

Alisema katika mechi hiyo Yanga, itawatumia wachezaji wake Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda na Didier Kavumbagu wa Atletico FC ya Burundi.

Mratibu huyo alisema Coastal Union nayo itapata nafasi ya kuwatambulisha wachezaji wake wapya akiwemo Jerry Santo aliyewahi kuichezea Simba, Job Nsa na Atupele Green.

Athuman alisema Coastal Union ambayo kwa sasa inanolewa na Juma Mgunda, aliyerithi mikoba ya Jamhuri Kihwelu 'Julio', imepania kufanya kweli katika mechi hiyo na kuidhihirishia Yanga kwamba wapo vyema.

Alisema maandalizi ya mechi hiyo tayari yamekamilika, kinachosubiriwa ni siku ifike ili mashabiki wa soka wapate burudani ya nguvu.


No comments:

Post a Comment