22 August 2012

Serikali yapewa siku saba kulifungulia MwanaHalisi


Rehema Maigala na Stella Aron

SIKU chache baada ya Gazeti la MwanaHalisi kufungiwa kwa muda usiojulikana, Serikali imepewa siku saba kuhakikisha inalifungulia bila masharti yoyote kwa sababu ya kuandika habari zinazomuhusu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dkt. Steven Ulimboka.

Mwenyekiti wa Kamati ndogo iliyoundwa baada ya Serikali kulifungia gazeti hilo, Bw. Marcossy Albanie, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kama Serikali itashindwa kufanya hivyo, asasi mbalimbali za kiraia zitaitisha maandamano makubwa nchi nzima kupinga hatua ya kufungiwa gazeti hilo bila sababu za msingi.

Aliongeza kuwa, maandamano hayo yataitishwa na wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu pamoja na waandishi wa habari kwani sheria iliyotumika kulifungia gazeti hilo ni kandamizi.

"Serikali imelituhumu gazeti hilo kwa kuchapisha habari ambazo zinakiuka vifungu vya sheria ya magazeti namba tatu ya mwaka 1976, habari iliyoandikwa inahusu kutekwa kwa Dkt.Ulimboka, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande,"alisema.

Bw. Albanie alisema Serikali imetumia mabavu kulifungia gazeti hilo kwani hawakutaka kusikiliza upande wa pili ambapo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, anafahamu sheria iliyotumika ni ya kikatili na imepitwa na wakati.


"Serikali itekeleze haraka suala hili ndani ya siku saba, asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Bw. Pinda ya kutaka wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu sheria ya magazeti hairuhusu ukataji rufaa kwa Waziri wa Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kutoa hukumu,"alisema.

Aliongeza kuwa, Bw. Pinda hakusema kama amepokea malalamiko ya gazeti hilo kuandika habari ya kichochezi hivyo hiyo ni njia mojawapo ya kukwepa wajibu wake.

"Serikali inashinikiza MwanaHalisi waende mahakamani wakati kesi nyingi zinacheleweshwa zikiwa huko hivyo hali hiyo itasababisha gazeti hili kutopata haki," alisema Bw. Albanie.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA), Bw. Tumaini Mwailenge, aliitaka Serikali kulishughulikia tatizo hilo haraka na kuondokana na sheria kandamizi kwa vyombo vya habari.

2 comments:

  1. Nafikiri cha msingi ni vyombo vya habari kuweka mgomo wa kuratibu na kuandika habari zozote zinazohusu serikali. Pasiwe hata napicha wala habari yeyote inyohusu serikali katika magazeti na radio, pia TV

    ReplyDelete
  2. JE HII HAITAKUWA KUMTISHIA BINADAMU NYAU ILI RAIS MKAPA HAKURUHUSU UHURU WA AINA HII MBONA NAYE ALIKUWA MWANDISHI WAHABARI.UHURU BILA NIDHAMU NI WENDAWAZIMU .

    ReplyDelete