22 August 2012
CEGODETA: Serikali ifunge akaunti Uswisi
Jesca Kileo na Jane Hamalosi
TAASISI ya Utawala Bora na Maendeleo nchini (CEGODETA), imeiomba Serikali kuwasiliana na Serikali ya Uswisi ili kufunga akaunti za wanasiasa na wafanyabiashara wa Tanzania ambao wanadaiwa kutorosha na kuficha fedha zao nchini humo.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bw. Thomas Ngawaiya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema taasisi hiyo imefadhaishwa na taarifa ambazo zimetolewa na baadhi ya wabunge juu ya wanasiasa na wafanyabiashara ambao wametorosha na kuficha fedha hizo sh. trilioni 11.6.
"Fedha hizi zinakaribia bajeti ya Serikali kwa mwaka mzima, wabunge wamedai upo ushahidi wa madai yao kutokana na taarifa ambazo zimetolewa na Global Financial Integrity.
"Pia wanadai kupata taarifa za siri kutoka Benki Kuu ya Uswisi, ambayo imeonesha kuna dola za Marekani zipatazo 315 sawa na sh.bilioni 478 za kitanzania ambazo zimefichwa nchini humo," alisema.
Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa, kuna baadhi ya wanasiasa ambao hawana uchungu wala uzalendo bali kipaumbele chao ni kujitajirisha wao binafsi na familia zao.
"Hii ni sababu mojawapo inayoifanya Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, licha ya kuwa na rasilimali nyingi, hadi sasa asilimia 60 ya Watanzania wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku na mlo mmoja tu,"alisema.
Bw. Ngawaiya alisema fedha hizo zikirejeshwa nchini zitumike kuboresha sekta za elimu na afya kama ilivyofanyika katika fedha za rada na kuongeza kuwa, wote ambao itabainika wamehusika na hujuma hiyo bila kujali nyadhifa zao, wafikishwe mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi ili iwe fundisho kwa wengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
INAPOFIKIA MATAIFA MAKUBWA KAMA URUSI NA CHINA LICHA YA KUWA NA SHERIA YA KUUA MBONA WIZI UPO TENA MKUBWA HAINGII AKILINI KITAIFA KAMA TANZANIA KIWEZE KUFUNGA AKAUNTI HUKO USWISS USHAURI HUU NI SAWA NA WA NGUVU ZA GIZA NA KUDHIHIRISHA UWEZO WETU WA KUFIKIRI NI SIFURI .
ReplyDeleteSijui kama mtu angekuwa anajua kuwa akiweka fedha zake kwenye akaunti za benki fulani siri hiyo itatoka nje basi asingeweka na ingekuwa vema akatumia njia nyingine ya kuhifadhi fedha hizo labda kwa kuwekeza kwenye kujenga majumba na mahoteli mashule au miradi ya kuleta maendeleo
ReplyDeleteBenki za Uswisi ambazo ni kati ya benki aminifu sana sasa zimefikia kuuonysha Ulimwengu kuwa pamoja na uaminifu wao na kuweka fedha za mataifa mengi duniani lakini dunia ifahamu idadi ya wateja wao ili kufuatilia kwa makini ni wapi fedha hizo zilikopatikana.
Kwa maoni yangu ni sawa na mtu kuingiza fedha za madawa ya kulevya nchini na kuvuruga uchumi wan nchi kwa kuongeza inflation nk. Kwa benki za uswisi kuwa wawazi ni sawa na kutokuruhusu fedha zilizopatikana kwa njia haramu kuwepo kwenye akauti zao na ndiyo maana wapo tayari kushirikiana na nchi husika kuwaonyesha wateja wao ili nchi hizo zisuke au kunyoa kuwachukulia hatua wahusika.
Taarifa iliyotolewa na mheshimiwa Ngwaiya ni chachu kwa serikali inayosema haina fedha na huduma zake nyingi zimedorora kama Afya , Elimu nk
Kitendo cha kuwepo kwa Trilion za Tshs ambazo ni fedha za kutosha bajeti ya mwaka hakiwezi kuachwa bila kuzungumzwa kwani kwa kufanya hivyo tumehalalisha kuwa wateja hao walizipata toka kwenye mishahara yao halali nchini Tanzania
Wazo la Ngawiya kurudisha fedha hizo kwenye mfuko wa Taifa ni wazo zuri kwani kwa kutokufanya hivyo tunahalisha wizi kwa watendaji wote wa serikalini au sector za umma.
Tukio alilolifanya marehemu Sokoine na kusababisha watu kutupa fedha zao na mali zao baharini lilikuwa ni kuonyesha uchungu na nchi yake na baadaye kuanzishwa kwa sheria ya uhujumu uchumi.
Sasa sijui ile sheria imekwenda wapi na ni kwanini haitumiki hasa kwa hawa wenye kiasi kikubwa hivi cha fedha. Kwanini tunaoneana aibu kiasi hiki wakati wengine wanateseka. Mheshimiwa Raisi Kikwete hebu lishughulikie hili ili heshima yako iendelelee kuwepo. Mwalimu Nyerere ma Marehemu Sokoine walikubaliana kuwashughulikia wahujumu uchumi ndiyo maana hadi leo tunawakumbuka na tutaendelea kuwaenzi
Tusisahau kuwa maisha yetu ni mafupi sana malimbikizo haya ya fedha zilizotokana na uhujumu uchumi za nini .vilio vya wale waliozulumiwa kwa hila vimeshamfikia mwenyewe Muumba
Mungu ibarikai Tanzania