11 July 2012
Wanandoa wauawa kwa mapanga kama wanyama
Na Moses Mabula, Tabora
WATU wawili ambao ni mume na mke, Bw. Khalid Said (55) na mkewe Amina All (50), wameuawa kikatili kwa kukatwa mapanga katika Kata ya Ndevelwa, Manispaa ya Tabora.
Mauaji hayo yametokea jana saa moja usiku wakiwa nyumbani kwao baada ya kuvamiwa na watu wawili waliokuwa na fimbo pamoja na mapanga ambayo waliyatumia kuwakata sehemu mbalimbali za miili yao kama wanyama.
Akizungumza na Majira, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Bw. Suleiman Kumchaya ambaye alitembelea eneo la tukio, alisema Serikali itawasaka na kuwakamata watu waliohusika na mauaji hayo.
Alisema Serikali haiwezi kuvumilia unyama huo uendelee mkoani hapa ambapo vitendo hivyo lazima vikomeshwe kwani Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, imejipanga kukomesha ukatili huo.
“Naomba wananchi watoe ushirikiano ili wahusika wa mauaji haya waweze kukamatwa kama wanafahamika na kufikishwa katika vyombo vya sheriaa,” alisema Bw. Kumchaya.
Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi litawajibika kumlinda mtu yeyote ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watu hao kwani mauaji ya aina hiyo hayakubaliki kwenye jamii na kuongeza kuwa, hadi sasa polisi
wanamshikilia shemeji wa marehemu ambaye anasaidia uchunguzi.
Akizungumzia mauaji hayo, mtoto wa marehemu Bi. Zainabu Khalid (30) alisema alishuhudia watu wawili wanaume wakiwa wamepanda baiskeli na kuwatafuta wazazi wake.
“Niliwasikia wakisema wametumwa kuwaua wazazi wangu, walifanya hivyo, kupanda baiskeli na kutokomea polini, baada ya kufanikisha mauaji, tulipiga kelele na wanakijiji waliitikia wito kwa kufika nyumbani haraka,” alisema.
Alisema kabla ya mauaji hayo, kulikuwa na mgogoro wa shamba kati ya baba yake na mjomba wao ambaye mara nyingi ametishia kumpiga marehemu.
“Shamba hili lilikuwa la marehemu babu ambaye alimpa mama enzi ya uhai wake lakini mjomba aliwahi kusema lazima damu itamwagika,” alisema Bi. Khalid.
Jeshi la Polisi mkoani hapa limekiri kutokea mauaji hayo ambapo hivi sasa wanaendelea na uchunguzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
ama kweli watu wamekuwa hawana huruma na maisha ya wenzao ni nini kilichowafasibu wakawakatakata mapanga hao wa2 jamani kuweni na huruma, acheni roho za kigaidi kweli ni cku za mwisho, yesu akirudi hatawakuta watu wake kwani wengi wamekuwa cyo watu
ReplyDelete