23 July 2012

Mmiliki Mv Skagit, nahodha mbaroni *Maiti nyingine tano zaopolewa, sasa zafikia 73


Na Mohammed Mhina, Jeshi la Polisi-Zanzibar

JESHI la Polisi Zanzibar, linawashikilia wafanyakazi sita wa meli ya Mv Skagit akiwemo mmiliki wake Bw. Said Abdulrahman pamoja na Nahodha wa meli hiyo, Bw. Mussa Makame Mussa.

Wafanyakazi hao, wote wanaendelea kuhojiwa kutokana na ajali ya kuzama kwa meli hiyo na kusababisha vifo vya baadhi ya abiria wakati ikitoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar.

Mahojiano hayo yanafanyika katika Ofisi za Upelelezi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi mjini Zanzibar ambapo Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, ACP Yusuph Ilembo, amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Kamanda Ilembo alisema, Makachero wa jeshi hilo wanaendelea na uchunguzi ili kutafuta taarifa nyingine zinazohusu tukio hilo.
 
Hata hivyo, Nahodha wa zamu siku ya tukio la kupinduka kwa meli hiyo, Bw. Mussa alieleza kwa ufupi jinsi ajali ilivyotokea na namna alivyonusurika katika tukio hilo.

Alisema meli hiyo ilipigwa na dharuba na mawimbi yaliyoambatana na upepo mkali, ambapo yeye alinusurika kufa maji baada ya kuruka kwa kutumia mlango wa mbele na kuogelea kwa kujichanganya pamoja na abiria wengine walionusurika ambapo wote waliokolewa na vyombo vya uokoaji.

Wakati huo huo, wapiga mbizi wa vikosi vya ulinzi na usalama, jana wamefanikiwa kupata maiti nyingine tano akiwemo mwanamke mmoja na wanaume wanne.

Katika upekuzi wa maiti hizo, Makachero wa Polisi walibaini kitambulisho cha kupigia kura kutoka kwa mmoja ya mwili
wa marehemu kilichokuwa na jina la Philip John Busiya.

Marehemu huyo alizaliwa mwaka 1977, kwenye Kijiji cha Mapilinga, Kata ya Igokelo, Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza ambapo kupatikana kwa miili hiyo, kunaifanya idadi ya maiti kufikia 73 kutoka 68 ya awali.

Maiti nyingine 68 zilipatikana siku za mwanzo baada ya kutokea ajali hiyo ambapo kati ya hizo, 54 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi.

Maiti hiyo ilipewa namba 72 na nyingine nne kuzikwa katika makaburi ya pamoja yaliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar eneo la Kama ambalo pia limetumika kuwazika watu wengine waliokosa ndugu wakati wa ajali ya meli ya Spice Islander  iliyotokea Septemba 9,2011.

Kupatikana kwa miili hiyo, kumetokana na juhudi zinazoendelea kwa kushirikisha vikosi hivyo, wazamiaji wa kampuni binafsi na Mamlaka ya Bandari Zanzibar walipokuwa katika harakati za kutafuta meli hiyo ili kubaini kama kuna miili mingine iliyosalia.

Juhudi za kutaka kuiibua meli hiyo, zinaendele ambapo wazamiaji wa JWTZ, Polisi, KMKM, JKU, Bandari, kampuni binafsi na wale wa kujitegemea, wanaendelea na kazi ya kutafuta mahali ilipo ili kuona kama wataweza kupata miili mingine iliyonasa kwenye vyumba vya meli.

4 comments:

  1. hongera captain mussa kwa kujiokoa! tunafurahi kwa kutokukupoteza. fani hii inahitaji makepteni makini kama wewe........ mungu akupe afya nzuri ili uanze tena kazi yako.

    ReplyDelete
  2. Siwezi kukupongeza captain Mussa, ulitakiwa kuwasaidia abiria wako, kwa kuwapa maboya na kuwa sehemu ya uokoaji, kwa kuwaonyesha mlango uliotokea wewe ili nao watoke wajichanganye, inakuwaje wewe tena unayetegemewa unaruka kupitia mlango wa mbele na kuacha abiria wako. Nahodha mwema ni yule anayejaribu kuokoa wenzake na hata ikibidi kupoteza maisha.

    ReplyDelete
  3. wa tz.hatuishi kwa kufuata kanuni ambazo tumeziweka cc wenyewe ktk sekta nyingi tu co meli tu lakini kwa sababu za rushwa na baadhi ya viongozi kuwa wamiliki wa hivyo vitu basi tutaendelea kuhesabu maafa majanga makubwa kila cku.hao watendaji wamewekwa na hao wenye kusababisha hayo majanga kwa hiyvo hawawezi kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa kanuni za wanacho kisimamia

    ReplyDelete
    Replies
    1. Imefika wakati sasa udhibiti wa ukaguzi wa Meli uchukuliwe kipaumbele zaidi na serikali, kwani udhibiti wa Meli ni kuanzia na ukaguzi wa makini, pakiwa na mkaguzi aliobobea (competent)na mzalendo. Ukaguzi huangalia usalama wa chombo vifaa vya kujiokolea vifaa vya kuzima moto vifaa vya kuongozea meli, mashine zote za meli na vyeti vya maofisa wa meli na mabaharia. Nahodha aliesoma na kuhitimu kuongoza meli, hawezi kukubali chombo chake kizidishiwe idadi ya mizigo au abiria. Nahodha makini akiona hali ya hewa mbaya anajua wapi pa kuelekeza meli.Udhibiti wa meli kwa kufanya ukaguzi unaostahili na pakiwa na upakiaji unaodhibitiwa na unaozingatia usalama wa meli abiria na mizigo, (Port State control officer,passenger manifest)maafa kama haya yatapungua au kwisha kabisa.

      Delete