23 July 2012

CHADEMA wamvaa Jaji Werema


Na Goodluck Hongo

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederck Werema, ameagiza wabunge wawili wa chama hicho Bw. John Mnyika (Ubungo), na Bw. Tundu Lissu (Singida Mashariki), wafunguliwe mashtaka.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, ambaye pia Mwanasheria wa chama hicho, Bw. Mabere Marando, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema madai kuwa ujumbe mfupi wa simu uliotumwa kwa Mbunge wa Iramba Magharibi Bw. Mwigulu Nchemba ukitishia kumdhuru ambao unadaiwa kutumwa na CHADEMA si ya kweli. bali suala hilo limetengenezwa ili lionekane limefanywa na chama hicho.

“Mimi nina ushahidi wa mtoto wa kiongozi mmoja aliyekwenda nchini Islael kununua mtambo kutoka Kampuni ya Nice System wenye uwezo wa kuingilia mawasiliano yako kwa kilomita tano na kuonesha umetuma ujumbe fulani ingawa si wewe.

“Tuna ushahidi wa kutosha kuwa Jaji Werema ameagiza kufunguliwa mashitaka wabunge wetu baada kufanya uchunguzi wa kina na kugundua kuna mchezo umefanyika ili ionekane ujumbe huo umetoka kwa wabunge wa CHADEMA, tupo tayari kuvaa majoho kwa ajili ya kesi hii,” alisema Bw. Marando.

Aliongeza kuwa, chama hicho kinasikitika kutokana na muda unaopotea katika mambo ya kipuuzi kama hayo na kwamba hata  wakiwauwa, kuwatesa na kuwafanya chochote, nguvu ya CHADEMA itaendelea kukua.

Alisema Sheria za Bunge zinataka mbunge kujadili mambo ya siri na ya wazi lakini wabunge wa CHADEMA wakitaka kujadili masuala ya Dkt. Steven Ulimboka, wanakatazwa kwa madai kesi hiyo ipo Mahakamani lakini wabunge wa CCM wanaruhusiwa.

“Watanzania ni mashahidi, wanaona ni jinsi gani viongozi wa CCM wanavyowapinga wabunge wetu ambao wanatetea wananchi, Jeshi la Polisi linakwenda kumkamata mtu kichaa na kulisingizia Kanisa.

“Watu wakitaka kulijadili hili wanaambiwa lipo mahakamani lakini akina Nchemba wanalizungumza bila kuzuiliwa, kwa hili la ujumbe ufupi wa maneno tupo tayari kuvaa majoho,” alisema.

Wakati huo huo, chama hicho kimetoa salamu za pole kwa wananchi wa Zanzibar na Serikali kwa ujumla kutokana na tukio la kuzama kwa meli ya Mv Skagit, kusababisha vifo, majeruhi na upotevu wa mali za abiria.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Willibroad Slaa, alisema CHADEMA inaungana na Watanzania wote kupeperusha bendera nusu mlingoti kwa siku tatu ambapo Mbunge wa chama hicho Bw. Vicenti Nyerere (Musoma Mjini), yupo Zanzibar akiungana na wananchi kuhusu tukio hilo.

1 comment:

  1. CHADEMA acheni kuwaongopea wa tz mmezidi kutaka umaarufu matokeo ni hasara mna spend mamilioni kuendesha kampuni yenu. lakini dalili ya kupata faida ni ndogo kwa sababu wenzenu wanatumia uzoefu. wanawatega kwa kukosa kwenu uzoefu mnanasa. kisha mnaanza kulalamika mtambo kutoka israel.wakati huo uko mahakamani na umaarufu kwisha muda pesa vinapotea.fanyeni siasa makini acheni visingizio ili mueleweke kwa wananchi

    ReplyDelete