26 June 2012
Majambazi wavamia TCU, waiba
Stella Aron na Rehema Maigala
KUNDI la watu wanadhaniwa kuwa majambazi, wamefanya uporaji wa mali mbalimbali katika ofisi za Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), baada ya kuwalewesha walinzi wa Kampuni ya Bulwark kwa kuwapa chakula kinachosadikika kuwa na dawa za kulevya.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tukio hilo limetokea juzi saa tatu usiku na kufanikiwa kuiba kompyuta, televisheni, printa na nyaraka mbalimbali.
“Baada ya majambazi hawa kuwalewesha walinzi, waliingia ndani ya ofisi hizi kirahisi, sisi tunaamini hawa ni wezi, hili si tukio la kwanza kwa walinzi kupewa vyakula na watu wasiofahamika.
“Tunawaomba walinzi wa kampuni zote kuacha tabia kupokea vyakula kwa watu wasiofahamika,” alisema Kamanda Kenyela na kuongeza kuwa, walinzi hao wamelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala chini ya ulinzi wa polisi.
Kamanda Kenyela alisema, polisi wamefanikiwa kukamata bunduki moja iliyokuwepo eneo la tukio ambayo inadhaniwa iliachwa na majambazi hao.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa TCU, Bw. Edward Mkaku, alisema kundi la watu hao liliingia ndani ya geti kubwa baada ya kukata kufuli kwa kutumia gesi, kuvunja makufuli ya vyumba 32 na kuiba vitu mbalimbali.
Alisema kuwa baada ya kuingia ofisini asubuhi, walimkuta mlinzi mmoja akiwa nyuma ya geti na mwingine nyuma ya jengo wote wakiwa hawajitambui ambapo kutokana na wizi huo, ofisi hizo hazikuweza kutoa huduma yoyote.
Aliwataka wanafunzi wanaotaka kujiunga na chuo, kuendelea na utaratibu wa kuomba kwani nyaraka zote muhimu zipo. Baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo ambao wamezungumza na Majira, walisema yawezekana watu hao ni majambazi wanaotumia silaha kufanya matukio mbalimbali.
“Hawa ni majambazi kwani licha ya kuja na bunduki, bado walijiamini ndio maana wakavunja ofisi mbalimbali wakiamini watapata fedha badala yake wameambulia vitu vingine,” alisema mfanyakazi mmoja wa ofisi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Wakati huo huo, taarifa zilizotufikia wakati tukienda mtamboni, zinasema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata nyaraka mbalimbali zilizoibwa katika ofisi hizo.
Kamanda Kenyela alisema, polisi walifanya msako mkali na kufanikiwa kukamata baadhi ya vitu kama barua za maombi za wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali, funguo za magari, vitabu vya taarifa za wanafunzi kutoka benki na televisheni moja aina ya Sumsung ambayo ilisahaulika katika eneo la tukio.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment