26 June 2012

Mganga wa kienyeji ajipaka kinyesi polisi


Na Said Hauni, Lindi

MKAZI wa Kijiji cha Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Bw. Abdurahamani Makame, ambaye ni mganga wa kienyeji maarufu “Daktari Majoka”, mwishoni mwa wiki aliharibu hali ya hewa kwenye Kituo cha Polisi mjini Lindi baada ya kujipaka kinyesi mwilini.

Habari zilizothibitishwa na baadhi ya askari polisi kituoni hapo pamoja na wananchi waishio jirani na kituo hicho (majina tunayo), zinasema Bw. Makame alifanya kituko hicho Juni 19 mwaaka huu.

Wakizungumza na Majira, baadhi ya askari waliokuwa zamu siku hiyo, alisema Bw. Makame aliamua kujipaka kinyesi mwilini ili kujinasua mikononi mwa polisi baada ya kufanya utapeli kwa wakazi wa Kata ya Mtama, wilayani hapa.

Walisema Dokta Majoka alifikishwa kituoni hapo baada ya wakazi wa kata hiyo kutoa taarifa polisi kuhusu vitendo vyake kuwatapeli wananchi akidai kuwa na uwezo wa kuwatambua na kutoa uchawi.

Waliongeza kuwa, baada ya kufikishwa kituoni na kuwekwa mahabusu, aliamua kujisaidia haja kubwa, kuchukua kinyesi chake na kukipaka mwili mzima ambapo hali hiyo ilileta tafrani kubwa kituoni hapo.

“Pamoja na huyu jamaa kutumia mbinu hii, haikuweza kumsaidia kutoka mikononi mwa dola, baada ya muda kupita aliomba msaada wa maji ili aweze kunawa na kupiga deki ndani ya chumba alichokuwa amehifadhiwa.

“Yeye alifanya vile akiamini pengine ataachiwa, sisi tuliendelea kuvumilia harufu ya kinyesi,” walisema askari hao.

Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa kata hiyo walisema Dokta Majoka amekuwa akiwanywesha baadhi ya watu dawa zake ili wawe na uwezo wa kuwabaini wanaojihusiha na uchawi.

Walisema watu waliokunjwa dawa hizo, wameweza kupata madhara mbalimbali ya kiafya kama kuumwa na kichwa na kupoteza fahamu.

“Mimi alininywesha dawa yake, kunitangaza mchawi na kuninyoa nywele kichwani kwa nguvu,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo.

Mkazi mwingine alisema Dokta Majoka alikwenda nyumbani kwake, kumpatia dawa ya kunywa, kuchimba Shimo na kufukia dawa zake ambazo zilimfanya azimie na kupoteza fahamu.

Wakionekana kukerwa na vitendo vya utapeli vinavyofanywa na Dokta Majoka, wakazi hao wameiomba Serikali iwakamate na kuwafikisha mahakamani waganga wote wanaojifanya kuwa na uwezo wa kutoa uchawi wakati hawana.

Mwenyekiti wa Serikali Kijiji cha Majengo 'B, Bw. Busara Mohamedi, aliiomba Serikali iwajibike kupinga vitendo hivyo ambavyo vinafanywa na waganga matapeli.

“Jambo la kushangaza hawa waganga wanaibuka wakati wa mavuno, kipindi cha ukame hawaonekani, Serikali iufanyie uchunguzi wa kina unga unaotumiwa na waganga kuwalisha wananchi ili kujua usalama wake,” alisema.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, George Mwakajinga, amewaomba
wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kukomesha vitendo hivyo vya kitapeli.

Vitendo vya watu kujifanya waganga wa kienyeji wenye uwezo wa kutoa uchawi katika nyumba mbalimbali vimekuwa vikijitokeza mara kwa maara licha ya baadhi yao kukamatwa na kufungwa kutokana na tabia hiyo.

No comments:

Post a Comment