26 June 2012
DPP kufikishiwa jarada maiti iliyopotea
Rehema Maigala na Stella Aron
SAKATA la maiti ya mtoto mchanga iliyopotea katika Hospitali ya Mwananyamala Dar es Salaam, limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kulifikisha suara hilo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Bw. Eliezer Felesh, kwa uchunguzi zaidi.
Familia iliyopotelewa na maiti hiyo, imechukua uamuzi wa kufungua kesi ya madai kutokana na utata wa suala hilo.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, kaka wa baba aliyepotelewa na maiti, Bw. Salimu Issa, alisema suala hilo imeamuliwa lifikishwe kwa DPP.
“Polisi wamefanya uchunguzi lakini wamefikia hatua ya kupeleka faili kwa DPP, uongozi wa hospitali hii ulisema siku ya tukio kulikuwa na wanawake wawili wanaofanana majina (Elizabeth), ambao walijifungua watoto waliofariki,” alisema.
Aliongeza kuwa, kutokana na mkanganyiko huo uongozi wa hospitali hiyo uliamua kuwatafuta lakini walipojieleza, walidai kuchukua maiti ya mtoto wa kiume na kuizika.
“Sisi maiti yetu ni ya mtoto wa kike ambayo tunaitaka ili tukamzike kwa kuzingatia misingi ya dini na mila zetu, tunataka kujua nani aliyechukua maiti hii bila idhini yetu,” alisema Bw. Issa.
Alisema shemeji yake Bi. Salha Ibrahimu (20), mkazi wa Mburahati, alijifungua mtoto mfu Juni 21 mwaka huu, saa nne asubuhi.
Bw. Issa alisema, baada ya kupata taarifa za shemeji yake kujifungua mtoto mfu, walikwenda hospitali saa sita mchana kuchukua mwili wakauzike lakini walishangazwa na uongozi wa hospitali kudai maiti hiyo haionekani.
“Tulianza harakati za kuutafuta kwa kushirikiana na viongozi wa hospitali hadi ilipofika saa moja usiku maiti haikupatikana hivyo tuliamua kufungua kesi Kituo cha Polisi Osterbay na kupewa RB namba OB/RB/11351/2012,” alisema Bw. Issa.
Awali Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Sophinias Ngonyani, alikiri kuwepo kwa utata huo na kusema maiti hiyo haijulikani ilipo na kuitaka familia hiyo kufungua kesi polisi.
Dkt. Ngonyani aliongeza kuwa, mtoto huyo alizaliwa akiwa mfu na baada ya muda walipotaka kumkabidhi kwa familia yake, maiti hiyo haikuweza kuonekana.
“Muuguzi aliichukua maiti ya kichanga na kuipeleka wodi ya wazazi lakini baada ya hapo, hatufahamu ilipotea katika mazingira gani lakini suala hili tumewaachia polisi,” alisema Dkt. Ngonyani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment