26 June 2012
Amchinja mkewe kwa wivu wa mapenzi
JESHI la Polisi mkoani Dodoma, linamshikilia, mkazi wa Morisheni, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, Bw. Daniel Lusega (42), kwa tuhuma ya kumchinja mke wake na kumuua.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Zelothe Stephen, alisema tukio hilo limetokea Juni 25 mwaka huu, saa mbili asubuhi, katika eneo la Morisheni Kata, wilayani hapa.
“Mtuhumiwa alikwenda kuripoti mwenyewe Kituo cha Polisi wilayani Kongwa na kueleza wazi kuwa amemchinja na kumuua mke wake kwa sababu hamsikilizi,” alieleza Kamanda Stephen.
Alisema mtuhumiwa alikwenda kituoni hapo akiwa na barua iliyoeleza madai yake dhidi ya marehemu mkewe ambayo ameikabidhi kituoni.
“Katika barua hii, mtuhumiwa alimwandikia Ofisa Usalama wa Wilaya ambapo mwanamke aliyeuawa anaitwa Bi. Telophena Machimo (34), ambao wote kabila lao ni Wakaguru.
“Marehemu ni mkazi wa Morishoni na kazi yake ni kuuza mgahawa, askari walikwenda kukagua eneo la tukio na kukuta marehemu amechinjwa kwa kukatwa koromeo, kisu kilichotumika kufanya unyama huo na dimbwi la damu,” alisema.
Kamanda Stephen alisema, chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kwani mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kutembea nje ya ndoa bila kupeleka matumizi nyumbani.
Aliongeza kuwa, mtuhumiwa ana historia ya ugonjwa wa akili kwa mujibu wa maelezo ya ndugu zake na viongozi wa kijiji katika eneo hilo.
Mtuhumiwa amekamatwa na anashikiliwa kwenye Kituo cha Polisi wilayani hapa na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo
mkabili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment