29 May 2012

Watanzania washauriwa kutumia mkutano wa AfDB kujitangaza


Pamela Mollel na Jane Edward, Arusha

WATANZANIA wametakiwa kujitangaza kiuchumi kupitia mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ulioanza jijini Arusha ambao umewajumuisha marais sita wakiwemo magavana wa nchi mbalimbali za Afrika.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Dodoma Bw. Juma Mwapachu mjini hapa ambapo alisema kuwa hiyo ni fursa ya pekee kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika mkutano huo.

Bw. Mwapachu alisema kuwa mkutano huo ni muhimu kwa nchi ya Tanzania na unawajumuisha watu mashuhuri na si vikao vya Magavana tu pia Umoja wa Mabenki ya Biashara ya Afrika pamoja na vyombo vya habari mashuhuri.

Aliongeza kuwa katika mkutano huo pia kuna vyombo vya kupima ubora wa uchumi wa nchi mbalimbali na mfano Tanzania uchumi wake umekuwa ukitolea mfano katika mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Alisema kuwa, kupitia Benki hiyo pia wameweza kufadhili ujenzi wa miundombinu ya Barabara ya Namanga hadi Arusha na bado wapo mbio kuhifadhili barabara ya Moshi hadi Holili.

“Kweli uchumi wetu unabadilika kiharaka sana na ukitazama mtikisiko wa kiuchumi 2008-009 ambao kweli kuna nchi ambazo zimetikiswa kiuchumi," alisema Bw.Mwapachu

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini Tanzania Bw.Richard Kasesera alisema kuwa ni fursa adhimu ya kukuza uchumi kwa Mkoa wa Arusha na kuvitaka vyombo vya habari kuwa chachu ya kutangaza uchumi wa Tanzania wakati huu mkutano unapoendelea.

Aliongeza kuwa ni jambo la muhimu kwa vyombo vya habari kuelezea matatizo ya kiuchumi na kuacha kuzipa kipaumbele habari za vurugu za Zanzibar za vikundi vichache kwckuwa kufanya hivyo ni kuwanyima Watanzania kupata taarifa sahihi na kuwatia hofu wahisani.

Mkutano huo wenye kauli mbiu 'Afrika katika Ulimwengu wa Utandawazi, Changamoto na Fursa' unafanyika kwa siku nne na kukusanya zaidi ya washiriki 2,000.

1 comment:

  1. Ushauri huu ungetolewa miezi mitatu kabla ya mkutano kuanza!?

    ReplyDelete