30 May 2012
Kocha Stars awaota Drogba, Toure
Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen amesema uwezo binafsi wa wachezaji Didier Drogba na Yahya Toure wa Ivory Coast utawapa wakati mgumu katika mechi ya Jumamosi itakayopigwa jijini Abidjan.
Mbali na hilo, Kim ameahidi kufa au kupona pindi watakapokutana nao licha ya kwamba wapinzani wao wana wachezaji wengi wanaocheza ligi kubwa barani Ulaya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kim alisema anaiheshimu Ivory Coast kutokana na aina ya wachezaji iliyonayo, lakini kikubwa katika mechi ya Jumamosi atahakikisha wanacheza soka la uhakika.
"Nadhani hakuna asiyewajua akina Drogba, Toure na Kalou (Salomon) ni wachezaji wazuri Ulaya kutokana na kuwa fit kiuchezaji, hivyo tunatakiwa kujituma zaidi ili kupata matokeo mazuri," alisema Kim na kuongeza;
"Drogba na Toure wana 'massive indivudual powers' (nguvu kubwa binafsi) ambayo huweza kusababisha matokeo ya aina yoyote uwanjani na ndiyo maana ninawaheshimu kwa hilo."
Akizungumzia kuhusu upungufu wa kikosi chake, Kim alisema kina ukosefu wa nguvu (fitness) ambapo kwa muda uliobaki wa siku nne kabla ya kukutana na Ivory Coast, hawezi kurekebisha hilo ila atajitahidi wacheze soka la kiushindani.
Alisema watatumia mbinu za kulinda na kutawala mchezo ambapo mbinu hiyo itawafanya wawe na nafasi ya kutengeneza nafasi za kufunga.
Wakati huohuo, Kim alimwagia sifa kiungo Mrisho Ngassa kwa kusema sasa anaonekana kubadilika na kucheza kama alivyokuwa akicheza awali.
"Ngassa amefanya kazi kubwa katika mechi dhidi ya Malawi, kiwango kile sijakiona akicheze kwa muda mrefu hivyo ni mabadiliko makubwa kwake na ametambua thamani yake akiwa na timu ya taifa," alisema Kim.
Katika hatua nyingine, Kim aliliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuwa na mpango maalumu kwa wachezaji wa Ligi Kuu wawe na kiwango fulani cha nguvu (fitness) ili wakiwa Taifa Stars wasipate shida.
Kikosi hicho cha Stars kilipanga kuondoka nchini leo kwenda jijini humo kwa ajili ya mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014, zitakazofanyika nchini Brazil.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment