30 May 2012

Shule zajengewa uwezo wa kompyuta na vitabu


Na Eliasa Ally, Iringa

MBUNGE wa Jimbo la Kilolo mkoani Iringa Prof. Peter Msolla amekabidhi msaada wa kompyuta tatu na vitabu vya kiada, msaada wenye thamani ya shilingi milioni tisa uliotolewa na Kampuni ya Simu Airtel Tanzania katika shule tatu za sekondari jimboni humo.

Akikabidhi msaada huo katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Mazombe jana Prof. Msolla alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake katika kuendeleza elimu kwa wananchi wake.

Prof. Msolla alisema kuwa mbali ya kuwa shule hiyo ya Sekondari Mazombe haina umeme ila ametanguliza kompyuta hizo kama njia ya kuanza mkakati wa kuisaidia shule hiyo kupata umeme wa mionzi ya jua.

Alisema kuwa, shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kompyuta na kupelekea walimu kushindwa kuchapa mitihani ama kuandaa masomo yao kwa kutumia kompyuta na kuishia kuandaa mitihani na vipindi mbalimbali kwa kuandika kwa mkono jambo ambalo lilikuwa likikwamisha shughuli nyingine.

"Napenda kuipongeza sana...Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania kwa kusaidia maendeleo ya elimu katika jimbo langu, ndugu zangu wanafunzi na wazazi moja kati ya vipaumbele vyangu vilikuwa ni elimu na wakati nikiingia madarakani mwaka 2005 Kilolo ilikuwa na shule za sekondari tatu ila sasa tumepiga hatua na kuwa na shule zaidi ya 20, napenda kuwahakikishieni kuwa tutaendelea kupiga hatua katika maendeleo ya elimu," alisema.

Pia aliwataka wanafunzi kutumia vizuri nafasi hiyo waliyoipata kwa kuendelea kusoma kwa juhudi kubwa na kuwa katika dunia ya sasa elimu ndio kila kitu na bila elimu ni vigumu kuweza kufanikiwa

No comments:

Post a Comment