30 May 2012

Polisi na mahakama Handeni lawamani


Na Mashaka Mhando, Tanga

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamesema idara za polisi na mahakama zina wajibu mkubwa wa kumaliza tatizo la utoro na mimba shuleni badala ya kuwatupia lawama watendaji wa vijiji na kata.

Wakizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo, madiwani hao walisema idara hizo zimekuwa kikwazo kikubwa cha tatizo la mimba katika vijiji vingi wilayani hapa hatua ambayo inachangia kuongezeka siku hadi siku.

Diwani wa Kata ya Ndolwa Bw. Joel Mabula alisema wananchi wakishirikiana na watendaji wa vijiji wamekuwa wakiwakamata wahalifu wanaosababisha mimba kwa wanafunzi, lakini wanapofikishwa katika vyombo vya sheria, kesi hizo zimekuwa zikimalizika bila hatua zozote.

“Serikali za vijiji zina makosa gani jamani? Hadi tuwekeane nao mikataba…Mwenyekiti ningeomba sasa badala ya kuwabana viongozi wa vijiji Serikali Kuu ingetusaidia kuvibana hivi vyombo vya dola watu wakikamatwa wakifikishwa polisi na baadaye mahakamani, washitakiwa wanaachiwa,” alisema Bw. Mabula.

Diwani wa Kata ya Komkonga Bw. Ramadhani Kisatu alitoa mfano wa mtu mmoja (jina tunalo) kuwa alimpa ujauzito mtoto wa shule na kisha kwenda kuishi naye katika Mji wa Kitumbi.

"Walipomkamata na kumfikisha katika Kituo cha Polisi Kabuku, mshitakiwa huyo hakuchukuliwa hatua zozote na matokeo yake yupo huru hadi leo," alidai.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Hassain Mwachibuzi akifafanua juu ya muswada uliowasilishwa na mwanasheria wa halmashauri hiyo Bw. Mohamed Msemo alisema kuwa mkataba baina ya halmashauri na watendaji utakuwa na manufaa ya ufuatiliaji kwa kuwa watendaji hao watakuwa wakiitisha mikutano shuleni itakayokuwa ikifuatilia mienendo ya wanafunzi.


No comments:

Post a Comment