30 May 2012

NCCR-Mageuzi wavuna wanachama Mtwara



Na Mwandishi Wetu, Mtwara

CHAMA cha NCCR-Mageuzi mkoani Mtwara kimevuna wanachama wapya 2,517 katika Jimbo la Mtwara Mjini.

Takwimu hizo zilitolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri ya chama hicho Bw. Danda Juju alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.


Alisema kuwa, idadi hiyo imepatikana kuanzia Machi hadi Mei mwaka huu kutokana na jitihada za uhamasishaji ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa kitaifa na wa jimbo hilo.

“Chama kinazidi kushika kasi, tumekuwa tukivuna wanachama kila kunapokucha kwa sababu wananchi wanajua NCCR-Mageuzi ndicho chama makini kitakachoweza kuwakomboa.

“Nasema hivyo kwa sababu tangu Machi mwaka huu tulipofanya ziara ya kitaifa mjini hapa, tumeshaingiza wanachama 2,517 na idadi hii itazidi kushika kasi kwa sababu wananchi wa Mtwara wameshaamka, wananchi wa Mtwara wanataka mageuzi kutokana na kuichoka CCM,” alisema  Bw. Juju.

Kwa mujibu wa Juju ambaye pia ni Msaidizi Mkuu wa Mwenyekiti wa chama hicho Bw. James Mbatia alisema wanachama wanaojiunga na chama chao wanatoka Chama cha Wananchi (CUF), wengine Chama cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA.

“Hatutaki mzaha wakati huu, lengo letu ni kuhakikisha tunaifukuza CCM, tunataka Mtwara Mjini na Mtwara kwa ujumla wake, iwe ngome ya NCCR-Mageuzi kwani tunaamini hilo litawezekana kutokana na kasi tuliyonayo.

“Kama tuliweza kuibadilisha Kigoma na kuwa ngome ya NCCR-Mageuzi, kwa nini Mtwara na Mkoa wa Lindi ishindikane? Hilo haliwezekani, lazima tupambane hadi dakika ya mwisho na mbinu tulizotumia kuikomboa Kigoma ndizo hizo hizo tutakazotumia kulikomboa Jimbo la Mtwara Mjini,  Mkoa wa Mtwara na Lindi.

1 comment:

  1. Hongera sana NCCR. Hakika ninyi ni chama makini.Wakati wengine wanapiga blabla ninyi mnaongelea masuala yanayogusa maisha ya mtanzania, tena tofauti na vyama vingine hatujawasikia mkitumia lugha za matusi. Hizo ndizo siasa ambazo watanzania tunapenda kuona. Dumisheni mwendo huo.

    ReplyDelete