30 May 2012

Mashujaa yakomba hadi Meneja Twanga



Na Zahoro Mlanzi

BENDI ya muziki wa dansi ya Mashujaa, imetangaza rasmi kumnasa Meneja wa African Stars (Twanga Pepeta), Matrin Sospeter kujiunga na bendi hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa bendi hiyo, Charles Gabriel 'Chalz Baba' alisema ana furaha kuona kiongozi huyo amejiunga nao na ana imani itazidi kufanya vizuri katika anga ya muziki wa dansi.


Alisema amefanya kazi na kiongozi huyo kwa miaka sita akiwa Twanga Pepeta, hivyo anamfahamu vizuri kutokana na kujituma kwake kazini na hata nje ya kazi.

"Nina furaha kubwa kukutana tena na Sospeter katika kazi, nina imani tutaisukuma vizuri bendi yetu kutoka hapa ilipo na kusogea mbali zaidi ili kuzidi kuliteka soko la muziki wa dansi," alisema Chaz Baba.

Naye Sospeter alisema ameondoka Twanga kwa ridhaa yake bila kushawishiwa na mtu na kwamba anaishukuru familia ya Asha Baraka (Mkurugenzi wa Twanga Pepeta) kwa muda wa miaka 14 aliokaa nao katika bendi hiyo.

Alisema ameondoka Twanga si kwa lengo la kuipa wakati mgumu bendi hiyo, ila kwa ajili ya maendeleo ya muziki wa dansi ili kuongeza ushindani zaidi miongoni mwa bendi za muziki huo.

Meneja huyo alisema hana kinyongo na Asha, kwani ndiye aliyemfanya afike hapo na kwamba anawaomba mashabiki wa Mashujaa kumpa ushirikiano.

Wakati huohuo, Chaz Baba pia alizungumzia ujio wa nyimbo zao mpya ambazo ni Risasi Kidole, Dunia ya mola, Thamani ya mtu na Usidharau sifuri kwamba zitakuwa ni moto wa kuotea mbali hivyo mashabiki wao wakae mkao wa kula.

No comments:

Post a Comment