30 May 2012
Madega ajana katiba mpya Yanga
Na Suleiman Mbuguni
BAADA ya wanachama wa Yanga, kushinda vita ya kumwondoa Mwenyekiti wa klabu hiyo madarakani na kutakiwa kufanya uchaguzi mdogo Mwenyekiti aliyeondoka kabla ya uongozi huu, Imani Madega amesema ili klabu hiyo kongwe ifanikiwe ni lazima kufanyike marekebisho ya katiba.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Madega alisema katiba hiyo mpya ndiyo itakuwa suluhisho lililobaki pekee na ili klabu hiyo ifanikiwe ni lazima idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ipungue kutoka 13 hadi kufikia sita na Mwenyenyekiti atatakiwa kuwa na kura ya veto.
Alisema katika idadi ya wajumbe hao italazimika watatu wawe wa kuchaguliwa na wanachama, na mmoja ateuliwe na Mwenyekiti ambaye atakuwa na mamlaka kutokana na kuwa kura ya veto.
"Kwa hiyo baada ya marekebisho hayo wanachama watatakiwa kuwachagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, wajumbe watatu na mjumbe mmoja atateuliwa na Mwenyekiti ambaye atakuwa na kura ya veto.
"Kwa kufanya hivyo itakuwa imepunguza idadi kubwa ya wajumbe ambao wengine mara nyingi wanakuwa hawana kazi ya kufanya, isipokuwa wanasubiri mikutano ya klabu pekee litu ambacho kinaleta majungu wenyewe kwa wenyewe," alisema Madega.
Alisema baada ya mchakato huo, viongozi hao watatakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), ambalo hulipa viongozi wake akiwemo Rais Sepp Blatter.
Madega alisema hatua hiyo ya kuwalipa viongozi mishahara itaongeza uwajibikaji na kuondoa majungu, kwani haiwezekani mchezaji akawa wa kulipwa alafu kiongozi wa ridhaa.
"Haiwezekani hata kidogo kiongozi akawa wa kujitolea, alafu anahaha kumtafutia mchezaji mshahara wa sh. milioni 5, wakati nyumbani kwake hajaacha kitu hivyo ni lazima mfumo huu ubadilike kama kweli tunataka klabu zetu zipige hatua hatuwezi kuwa na mifumo miwili tofauti ndani ya klabu moja," alisema Madega.
Alisema hatua hiyo ya kuwalipa mishahara viongozi, itawaletea heshima kwa wanachama kwani hivi sasa kiongozi akiendesha gari anaonekana amelipata kupitia klabu, lakini kwa mfumo huu utaondoa dhana hiyo.
Kiongozi huyo alisema hatua nyingine muhimu ni kupunguza idadi ya wanachama wa kuingia katika mikutano ya klabu kwani sasa Yanga inakadiriwa kuwa na wanachama zaidi ya 10,000, ambao ni tatizo kama wakifika wote katika Mkutano Mkuu.
Madega alisema hakuna ulazima wa kuwakutanisha wanachama wote katika mikutano kwa kuwa si wote wanaochangia hoja, bali wengine hufuata mkumbo na kuanzisha majungu yasiyokuwa na maana.
"Si lazima wanachama wote wakaingia katika mikutano, wanaweza wakachaguliwa wawakilishi watatu kutoka kila tawi. Kwa mfano akawemo Mwenyekiti, Katibu na Mjumbe mmoja wa kuchaguliwa katika tawi husika.
Mfumo huo hautakuwa tofauti na vyama vya siasa ambavyo hutumia wajumbe maalumu kuingia katika mikutano yao kujadili mambo yao, kwani kama vingeamua kutumia wanachama wake wote ingekuwa ni tatizo kutokana na wingi wao nchi nzima," alisema.
Klabu hiyo inatarajia kufanya uchaguzi mdogo Julai 15, mwaka huu kutokana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kujiuzulu pamoja na Mwenyekiti wake Nchunga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment