29 May 2012

Kifukwe, Falcon, Karigo wanukia Yanga



Na Zahoro Mlanzi

SIKU 2 baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuitaka Klabu ya Yanga kufanya uchaguzi wa viongozi wapya Julai 15 mwaka huu, homa ya uchaguzi huo imeanza kupanda huku viongozi waliowahi kuiongoza klabu hiyo, Francis Kifukwe, Godson Karigo na Ahmed Falcon wakitajwa kuwania nafasi za juu.

Uchaguzi huo umelazimika kufanyika tarehe hiyo kutokana na wajumbe nane wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kujiuzulu huku mjumbe mwingine kufariki, hivyo kufanya nafasi zijazwe kwa ibara ya 28 ya katiba ya Yanga.

Viongozi hao waliamua kujiuzulu kutokana na kuona klabu hiyo ikiendelea na malumbano kati ya uongozi uliopo chini ya Mwenyekiti, Llody Nchunga na Wazee wa Baraza la Muafaka ambapo wazee hao walitaka Nchunga ang'oke baada ya kudai timu imemshinda.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili imezipata kutoka Makao Makuu ya klabu hiyo, Mitaa ya Twiga na Jangwani, zilieleza kwamba tayari kumeshaanza kufanyika kwa vikao vya siri kati ya viongozi mbalimbali waliowahi kuiongoza timu hiyo huku baadhi ya wanachama wakiwapigia chapuo waliowahi kuiongoza.

“Tayari vikao vimeshaanza na kuna baadhi ya wanachama wameanza kupanga safu zao za uongozi huku wengine wanataka kumrudisha Kifukwe, wengine mara Karigo au Falcon na kwamba inaonekana uchaguzi huu utakuwa na msisimko wa aina yake,” alisema kiongozi mmoja ambaye alijiuzulu katika uongozi uliopita.

Alisema kwa jinsi mwelekeo wa wanachama unavyoonekana, endapo mmojawapo kati ya waliotajwa akionesha nia ya kutaka kugombea hatakuwa na upinzani kwani inaonekana wanakubalika.

Gazeti hili lilifika klabuni hapo na kushuhudia kuwepo kwa vikundi vya wanachama wakiuzungumzia uchaguzi huo, huku wakiyataja baadhi ya viongozi waliopita lakini hawakuwa tayari kueleza zaidi mpaka Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo, iliyo chini ya Jaji John Mkwawa itakapotangaza rasmi.

No comments:

Post a Comment