29 May 2012
Tushirikiane kukomesha ukatili kwa wajawazito
WALI ilikuwa ikifikirika kuwa kazi ya uuguzi ni wito, hivyo kila anayefanyakazi hiyo ana sifa ya kuwa na ukarimu, upendo, upole na sifa zingine.
Kadri siku, miezi hadi mwaka inavyokwenda ndivyo sifa hizo zinavyotoweka.
Kutokana na ukosefu wa ajira nchini vijana wamejiamulia kujiingiza katika fani mbalimbali licha ya kutokuwa na sifa zinazostahili kuingia kwenye fani husika.
Hali hiyo imekuwa ikiendelea na kusababisha ukiukwaji wa baadhi ya maadili mbalimbali na kusababisha wananchi kuangamia na wengine kupoteza maisha.
Mwishoni mwa wiki iliyopita mwanamke Bi. Rukia Vulai, mkazi wa Magereza Manispaa ya Mtwara alijikuta akijifungulia ndani ya pikipiki ya miguu mitatu maarufu kama bajaji baada ya wauguzi waliokuwa zamu kumtolea lugha chafu.
Mwanamke huyo alifika kituoni hapo akiwa na uchungu mkali na kumuomba muuguzi mmoja amsaidie kwa kumkimbiza wodini kwa kuwa tayari dalili za kujifungua zilianza kuonekana baada ya chupa kuvunjika.
Badala ya muuguzi huyo kutakiwa kutoa huduma ya kwanza ili kuokoa maisha ya mama huyo anadaiwa kuanza kumtolea lugha chafu mwanamke huyo na kudai kuwa yeye hahusiki na kuwasaidia akina mama wajawazito.
Imedaiwa kuwa licha ya wagonjwa wengine waliokuwa pembeni kumbembeleza muuguzi huyo kumsaidia mama huyo hakuweza kufanya hivyo na badala yake aliendelea kumtolea lugha ya matusi mama huyo.
Kutokana na mabishano hayo kuendelea mgonjwa huyo aliweza kujifungua ambapo alisaidiwa na wanawake wengine ambao walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali na kujifungua ndani ya bajaji.
Kwa kweli suala hili limenisikitisha sana hata kama huyo muuguzi mama mjamzito alikuwa ni adui yake kwanza alitakiwa kumpa huduma kisha uadui wake auendeleze.
Wauguzi kama hawa wamekuwa vikwazo vikubwa katika vituo mbalimbali vya afya na hata hospitalini na kusababisha baadhi ya akimama kufariki ama watoto wao kutokana na kukosa huduma zinazostahili.
Imefika wakati sasa hakuna kuwaonea aibu wala kuwaachia wauguzi kama hawa kwa kuwa hawana huruma wala upendo kwa wagonjwa.
Malalamiko kama hayo yamekuwa yakiwapata akinamama wengi na kushindwa mahali pa kwenda kueleza kero hizo na hata wanapokwenda kutoa malalamiko hayo katika ngazi za juu huwaziba midogo kwa kuwadaganya kuwa kero hizo zitatatuliwa.
Hata hivyo hainiingii akilini ni kwanini wauguzi kama hawa waendelee kuwepo kwenye hospitali zetu na kuwa kero kwa jamii, ni bora kukawa na ofisi maalumu kwa ajili ya kupokea malalamiko ya wagonjwa na kufanyiwa kazi na kuchukuliwa hatua zinazostahili bila kuonea haya na kutangazwa.
Ukweli ni kuwa hivi vitendo vya kuwanyanyasa wanawake pindi wanapokwenda kujifungua vikomeshwe kwani vinawasababishia kuathirika kisaikolojia kutokana na kuwaza kubeba tena ujauzito na kuhofia kutukanwa.
Lakini pia matukio ya unyanyasaji kwa asilimia kubwa yamekuwa yakifanywa na wanawake ambao nao wapo katika mstari mmoja wa harakati za kumkomboa mwanamke kimapinduzi hivyo imefika wakati sasa tukashirikiana katika kukomesha vitendo hivyo.
Nionavyo mimi ni kuwa kama kuna wauguzi wa namna hii ni bora wapewe adhabu kali ambazo zitasababisha wauguzi wengine kuogopa na pia kuwepo kwa timu maalumu ya wafanyakazi wanaotembelea wodini na kusikiliza kero za wagonjwa na si kungoja kuletewa maofisini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

Matatizo kama haya yanatokea sana katika hospitali zetu za Serikali na Zahanati zake. Japo hujataja kama tukio hili limetokea katika Zahanati ya Serikali ama Private ila historia inaonyesha kuwa matukio haya yamekithiri sana katika Zahanati na hospitali za serikali. Tatizo kubwa ni kwamba viongozi hawawatembelei wagonjwa na kuongea nao kuhusu changamoto zinazowakabili - wanaishia kujifungia maofisi muda wote au hawapo kabisa kwenye vituo vyao vya kazi - utawakuta Bar!Wakipelekewa malalamiko - wanaishia kusema tutayafanyia kazi hakuna lolote linatokea - akitokea kulifanyia kazi kama ni mwanamke ametenda kosa basi atadaiwa rushwa ya ngono na biashara inaishia hapo.Nimetembelea hospitali nyingi na Zahanati za Serikali pamoja na zile za binafsi na misheni. Kuna tafauti kubwa sana katika kutoa huduma, wakati hawa wa Zahanati na Hospitali za Serikali wanalipwa kwa kodi zetu ndo wakorofi kupindukia. Ukiachilia mbali hilo la huduma - basi japo wawe na roho ya ubinadamu. Wajaribu kufikiria ingekuwa na wao au ndugu zao wanafanyiwa huo unyama wanaowafanyia wengine wangependwa kweli na hali hiyo? Tuache unyama, tuutumie ubinadamu wetu lol!
ReplyDelete