31 May 2012
January Makamba awafunda wananchi
Na Yusuph Mussa, Lushoto
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Bw. January Makamba amewataka wananchi wa Tarafa ya Mgwashi mkoani Tanga kutumia fursa mbalimbali ikiwemo kufanya biashara na Halmashauri mpya ya Bumbuli badala ya kuwaachia wageni waiuzie halmashauri hiyo hadi karatasi za ofisini.
Chanamoto hiyo aliitoa juzi wakati anahutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mgwashi Kata ya Mgwashi wilayani Lushoto na kuwaeleza wananchi kuwa kwa kupata halmashauri ni ushindi mkubwa kwani pamoja na kufanya biashara, lakini pia huduma za jamii zitaboreka.
"Nitashangaa kama nitaona hata biashara ya kuuza karatasi (shajala) mtawaachia watu kutoka Arusha. Sasa ni wakati wenu kufanya biashara na Halmashauri ya Bumbuli kwa kuchukua zabuni mbalimbali ili kuinua vipato vyenu," alisema Bw. Makamba.
Bw. Makamba aliwatahadharisha wananchi wa tarafa hiyo kuwa uteuzi wa yeye kuwa Naibu Waziri hauwezi kumaliza changamoto zao bali ataendelea kupigana kama Mbunge kuona kero mbalimbali zikipatiwa ufumbuzi moja baada ya nyingine.
"Jamani mimi nilipokuja hapa niliomba kazi ya ubunge. lakini sio uwaziri, hivyo nafasi yangu ya unaibu Waziri hauwezi kumaliza kero na changamoto zenu, bali kama nilivyopigana kama mbunge wenu wa kupata umeme tangu dunia iumbwe kwenye Tarafa ya Mgwashi.
"Ndivyo nitakavyo hakikisha barabara ya kutoka Mbelei hadi Mashewa inatengenezwa huku ikihamishiwa kutoka halmashauri kwenda TANROADS (Wakala wa Barabara) ambayo itawezesha kusafirisha mazao yenu, lakini pia
tatizo la maji linakwisha," alisema Bw. Makamba.
Awali, Ofisa Tarafa ya Mgwashi Bw. Moka Urban alimueleza Bw. Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli kuwa Kituo cha Afya Mgwashi kinaletewa dawa kama kata badala ya kituo cha afya, hivyo kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Bw. Urban alisema pia barabara ya kutoka Soni hadi Mgwashi sio nzuri, umeme bado haujafika kwenye vijiji vingi pamoja na kufika makao makuu ya kata ya Mgwashi na baadhi ya vijiji havina mawasiliano ya simu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment