23 May 2012

Ikwiriri sasa amani, mwafaka wafikiwa


Na Masau Bwire, Ikwiriri

MGOGORO mkubwa uliozuka Ikwiriri, Rufiji, mkoani Pwani kati ya wakulima na wafugaji kwa siku mbili mfululizo na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali umemalizika jana.

Utulivu katika eneo la Ikwiriri, umerejea baada ya Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi nchini, SACP Simon Siro, kutumia njia za kidiplomasia kutatua mgogoro huo.

Juzi jioni mwanadiplomasia huyo aliwaita na kukutana faragha kwa mazungumzo ya nini kifanyike ili kuleta amani katika eneo hilo kwa kushirikisha wananchi, viongozi wa dini, wanasiasa, baadhi ya viongozi wa Serikali, wafanyabiashara wakubwa na wazee mashuhuri.

Mazungumzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya saa nne, yalizaa matunda baada ya viongozi hao kukubali kuwatangazia wananchi kuacha vurugu na kuingia katika meza ya mazungumzo kati yao na Jeshi la Polisi ili kurejesha amani kwa njia salama.

Kamanda Siro aliwaambia viongozi hao kuwa, amani ya Ikwiriri haitapatikana kwa mabomu ya machozi au risasi za moto bali kwa njia ya mazungumzo ili kutafuta namna ya kuondoa kasoro zilizojitokeza na kusababisha vurugu hizo.

Viongozi hao walielewa somo la Kamanda Siro na kushiriki kuwaeleza wananchi umuhimu wa kuacha vurugu na kuwasihi washiriki mkutano wa hadhara kati yao na Kamanda Siro ambao ulifanyika jana katika Viwanja vya Africana mjini hapa.

Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na watu lukuki, wananchi wa pande zote mbili, wafugaji na wakulima walipewa nafasi ya kuzungumza kero zao na zikajadiliwa kwa pamoja chini ya usimamizi wa Kamanda Siro na kupatiwa ufumbuzi.

Wananchi kupitia mkutano huo, walikubaliana kuacha vurugu na kuweka maazimio matano ya nini kifanyike ili vurugu hizo zisijitokeze tena na kuazimia wafugaji warudi katika mipaka yao na wasivuke kuingia maeneo ya wakulima na viongozi wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo wawajibishwe.

Maazimio mengine ni kuhusu viongozi, polisi na watendaji wengine wa Serikali wanaojihusisha na rushwa wachukuliwe hatua, wafugaji waliohusika katika mauaji ya mkulima, Bw.Shamte Kawangala (80), wakamatwe na wafikishwe mahakamani.

Azimio lingine ni wananchi 53 waliokamatwa na kufikishwa mahakamani mashtaka yao yachunguzwe kwa kina na wale wasiohusika waachiwe na watakaobainika kuhusika sheria ichukue mkondo wake.

Akizungumza na Majira muda mfupi kabla ya kuondoka na helikopta kutoka eneo la mkutano, Kamanda Siro alisema maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo yameanza kufanyiwa kazi.

Baadhi ya wakazi wa Ikwiriri walipongeza hatua ya Kamanda Siro jinsi alivyoweza kushughulikia mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na maridhiano ya pamoja.








1 comment:

  1. Huo ndio msingi wa Jeshi la polisi linalotakiwa. Ni kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao. Matumizi ya nguvu, risasi na mabomu haviwezi kumaliza tatizo. Suala la msingi ni kutatua chanzo na sio matokeo. Polisi wanatakiwa kujua wapo kwa ajili ya wananchi na sio vinginevyo.

    ReplyDelete