24 May 2012
Milovan aipa wakati mgumu Simba
Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, Milovan Cirkovic ameiweka katika wakati mgumu timu hiyo baada ya kutaka kuongezewa mshahara kutokana na kuipa ubingwa timu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, jana Kamati ya Utendaji ya timu hiyo ilikuwa na kikao kizito na kocha huyo katika moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam kujadili hatma ya kocha huyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili ilizinasa kutoka katika kikao hicho Dar es Salaam jana kwa mmoja wa Wajumbe wa kamati hiyo, alisema Milovan ameomba kuongezewa mshahara pamoja na marupurupu mengine katika mkataba mpya watakaompa.
"Kikao bado hakijaisha kwani Milovan inaonekana yupo serious (makini) na kutaka kuongezewa fungu katika mkataba mpya ambao nao mpaka sasa tunavuta katika muda atakaofundisha timu hiyo," alisema kiongozi huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Gazeti hili lilimtafuta Ofisa Habari wa timu hiyo, Ezekiel Kamwaga kuthibitisha taarifa hizo ambapo alikiri kweli jana kulikuwa na kikao hicho kinachojadili mustakabali wa kocha huyo.
"Ni kweli hivi tunavyoongea kikao kinaendelea kati ya viongozi wa Simba na Milovan na kubwa zaidi ni katika suala zima la mshahara na muda atakaofundisha," alisema Kamwaga.
Alisema bado hawajasaini mkataba mpya na kocha huyo baada ya ule wa awali wa miezi sita kumalizika na kwamba baada ya kikao hicho kila kitu kitajulikana.
Akizungumzia suala la kusajili wachezaji wapya, Kamwaga alisema suala hilo lipo chini ya Milovan ambapo baada ya kusaini mkataba mpya ndipo atakapotoa mapendekezo ni wachezaji wangapi atawaacha na wangapi atawaongeza.
Pamoja na hayo, alisema Kamati ya Ufundi ya timu hiyo ambayo ipo chini ya Mwenyekiti, Ibrahim Masoud 'Maestro', ina uwezo wa kusajili wachezaji wapya lakini itawalazimu wakae chini kumshawishi Milovan juu ya mchezaji husika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment