14 May 2012

Gemini kudhamini mchezo wa Judo



Na Mwali Ibrahim

KAMPUNI ya Gemini  Corporation imejitokeza kudhamini mashindano ya taifa ya mchezo wa Judo yanayotarajiwa kufanyika Mei 26 hadi 27 Landmark Ubungo  Dar es Salaam.

Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha wachezaji kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watakaochuana kuwania ubingwa huo.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Yuil Tarverdyan alisema kutokana na mapenzi ya mchezo huo kampuni yake imejitokeza kugharamia mashindano hayo kwa mara ya pili ikiwa ni katika kugharamia gharama zote za mashindano.

Alisema, gharama hizo zitahusisha mahali pa kufanyia mashindano zawadi ambazo nifedha kwa washindi wa mashindano hayo.

Alisema, kutokana na chama cha Judo nchini (JATA) kwa sasa kuwa na viongozi wapya, anatarajia kufanya kikao cha pamoja na viongozi hao ambao tayari wameshawasiliana kuhusu udhamini huo, ambapo gharama za mashindano pamoja na zawadi atazitaja katika kikao hicho.

Alisema licha ya kuwa na mahusiano mazuri na uongozi uliopita hakusita kuacha kudhamini mchezo huo kutokana na mapenzi yake katika mchezo huo ambao pia huchezwa nchini kwao Ujerumani.

Kwa mujibu wa  aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Kashinde Shaaban aliyezungumza kwa simu alisema wanaitambua kampuni hiyo kutokana na kujitokeza kuwadhamini wakati wa uongozi wao, ambapo kwa sasa kiongozi huyo amefungiwa maisha.

"Alinipigia kutaka kudhamini kutokana na kufahamiana na uongozi wetu kipindi hicho, lakini nilimfahamisha kuwa sipo tena madarakani na kumtaka kuendeleza udhamini huo kwa viongozi waliokuwepo madarakani sasa," alisema Kashinde.


No comments:

Post a Comment