05 April 2012

Wakulima washauriwa kuongeza thamani ya korosho

Na Godwin Msalichuma, Kilwa
WAKULIMA wa korosho wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi, wamekitaka chama
kikuu cha ushirika mkoani humo, Ilulu kutenga korosho kwa ajili ya
kubangulia  ili kuziongezea thamani ya zao hilo na zingine kuzitafutia soko nje ya nchi.
Hali hiyo itasaidia kuacha  kutegemea wanunuzi wa kati ambao wengi wao ni wababaishaji  na wanachangia soko la zao hilo na hivyo kusababisha mkulima kukosa malipo kwa wakati na kuendelea kulima kilimo kisicho na tija.

Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na wakulima hao waliokutana katika
mkutano wa wadau wa kilimo ulioitishwa na shirika lisilo la kiserikali
la kimataifa la Action Aid Internainal Tanzania (AAIT) ikiwa ni sehemu
ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha na kukuza kilimo cha zao hilo
wilayani humo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha
maendeleo ya wananchi mjini Kilwa masoko.

Walisema ili kuondokana na ubabaishaji unaofanywa na wanunuzi wa kati
ni vyema Ilulu ikatafuta soko la zao hilo nje ya nchi na kuuza ,moja
kwa moja kwa wanunuzi wakubwa mara baada ya kukusanya korosho kutoka
kwa wakulima na kuachana na utaratibu wa sasa ambapo chama hicho
kinawauzia wanunuzi wa kati ambao nao wanaenda kuuza kwa wanunuzi
wakubwa wanauza nje ya nchi.


“Mfumo wa ununuzi unaotumika ni mzuri lakini linapokuja suala la soko
ndio tatizo linapoanzia hapo…tunadhani ili kuondokana na tatizo hili
ni vyema chama chetu kikuu kikatafuta soko nje ya nchi…lakini pia kiwe
na mipango madhubuti ya kubangua angalau kiasi kidogo ili kuongeza
thamani korosho zetu”, alisema Bw.Yusufu Mcheni Mwenyekiti wa Chama
cha Msingi cha TAPWA.

Naye Bw. Athumani Kingolopi wa Chama cha  Msingi Ujirani Mwema ,
alisema kuwa ununuzi  ulikwenda  vizuri mwaka jana chini ya mfumo wa
stakabadhi ghalani na kuwa  mfamo mzuri wa kuigwa, lakini mwaka huu
wanunuzi waligoma kununua kwa bei nzuri mnadani na hivyo kuyumbisha
wakulima ambao wengi wao hadi leo hawajalipwa malipo yao ya pili.

“Kwa maoni yangu naona ni bora tutenge kiasi fulani kwaajili ya
kubangua na zinazobaki zikuzanywe na kuuzwa moja kwa moja nje ya nchi
ili kuondokana na tatizo hili na kumuongezea mkulima kipato…hawa
wanunuzi wa kati wanatuyumbisha”, alisema Bw. Kingolopi.

Awali Mkuu wa Idara ya Kilimo na Usalama wa Chakula kutoka Action aid
Makao Makuu, Bw. Elias Mtinda, alisema kuwa shirika hilo lipo tayari
kuwadhamini wakulima hao ili kupata mkopo kutoka vyombo vya fedha
kwa ajili ya kununulia mashine za kubangulia korosho zao.

2 comments:

  1. Serikali imekwisha uza au kuvitelekeza viwanda vya kubangua Korosho. Hiyo thamani itaongezwaje? Viongozi acheni unafiki. Au ni kwa sababu Wa Vietnam waliwa cheka kupitia Semina ya REPOA ndio maana mnakumbuka shuka asubuhi?

    ReplyDelete
  2. Viwanda viliuzwa kwa watubisafsi ili kuongeza efficiency baada yakuona serikali imeshindwa kuviendeleza kutokana na tabia mbaya ya wizi wa maliza uma. Hiyo ndiyo ilikuwa principle objective lakini nao sekta binafsi walionunua kumbe wanatabia ya ulafi wakageuza viwanda kuwa magodauni. Kwanza walinunua kwa tama tu hawakuwa na uwezo wakuendeleza shughuli za kuongeza thamani hizo korosho.

    Tutafute suluhusisho la tatizo na tusiendelee na kulaumiana maana nasi kwakulaumu serikali tumezidi badala ya kuona lengo zuri la Serikali ilikuwa ni nini.

    ReplyDelete