05 April 2012

Utamaduni wa kutoa rushwa sasa tuukatae

TATIZO la rushwa nchini lipo katika sekta mbalimbali lakini hali hiyo haina maana kuwa inakubalika katika jamii.
Ukweli ni kwamba, rushwa haikubaliki kutokana na madhara yake ndio maana Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

Rushwa inaathiri maendeleo ya mtu binafsi, familia, Taifa na kushusha hadhi ya mtoaji na mpokeaji. Rushwa inachangia kupindisha kanuni za maadili wakati wa kutekeleza majukumu kwa maslahi ya umma, mtu au kikundi fulani.

Vitendo hivyo vinajumuisha matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha baadhi ya viongozi wa umma na sekta binafsi, kutumia madaraka waliyonayo kinyume cha sheria ili kujinufaisha.

Rushwa 'imebatizwa' majina mengi, wengine huiita mlungula, kitu kidogo, shati la mikono mirefu au zawadi.

Watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, wanawanyima wananchi mategemeo ya kuwa na maisha bora, kuwakosesha elimu, huduma bora za afya, chakula, maji na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Sisi tunasema kuwa, rushwa ni wizi dhidi ya Taifa na wananchi ambao wanategemea maisha bora, inachochea makosa ya jinai yanayovuka mipaka, kuvunja amani na utulivu.

Rushwa ina madhara makubwa kiuchumi kwa lugha nyepesi ni uovu unaowavunja moyo Watanzania na wafanyabiashara ambao wangependa kuwekeza nchini.

Inaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wakati mwingine husababisha kupungua ubora wa bidhaa ambazo huzalishwa viwandani.

Imani yetu ni kwamba, rushwa husababisha mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kupungua hivyo kupuguza uwezo wa kutoa huduma kwa wananchi kutekeleza malengo ya kuboresha maisha yao na miundombinu ya nchi.

Uovu wa rushwa unachangia kuongeza umaskini katika jamii, kuathiri ubora wa elimu na sekta nyingine nchini. Rushwa inaweza kusababisha mgonjwa asipone haraka au kupoteza maisha kama atakataa au kukosa kile alichodaiwa kukitoa.

Tukifikia kiwango cha kuibubali rushwa kama sehemu ya utamaduni wetu katika vyombo vya sheria, waathiriwa wataamua kujilinda wenyewe kwa kuchukua sheria mkononi hivyo kuharibu sifa ya amani na utulivu tulionao.

No comments:

Post a Comment