05 April 2012

Majambazi yavamia viongozi wa kanisa

Na Said Hauni, Lindi
WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia makazi ya viongozi wa dini ya Kikristo Parokia ya Nyangao Wilaya na Mkoa wa Lindi huku wakipora fedha taslimu sh. milioni tano.

Pia inadaiwa licha ya kupora fedha hizo viongozi hao, ilidaiwa walijeruhiwa watu wanne wakiwemo viongozi wawili na walinzi wao wawili kwa kuwacharanga mapanga sehemu mbalimbali ya miili yao.

Habari kutoka Kata ya Nyangao ambazo zilithibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa zilieleza kuwa tukio hilo lilifanyika Machi 30, mwaka huu majira ya saa 6:45 za usiku.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Bw. George Mwakajinga alisema katika tukio hilo watu watatu kati ya hao walishambuliwa kwa kupigwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao wakati mmoja alifungwa kamba na kutupiwa kwenye shimo la taka.

Bw. Mwakajinga aliwataja walioshambuliwa kuwa ni ni, Paroko Housiager Hugo (74) na Padri Michael Mrope (75), Bw. Victor Hanga (58) na Joseph Mathias (45) ambao ni walinzi wa nyumba za viongozi hao.

Alisema, Bw.Hugo ambaye kwa sasa amelazwa Hospitali ya Mision ya Ndanda iliyopo Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara alipigwa mapanga kichwani na mbavuni ambapo, Bw. Hanga ambaye ni mlinzi pia alijeruhiwa na panga kichwani na kulazwa Hospitali Teule ya Nyangao.

Pia aliongeza kuwa Padri Mrope alishambuliwa kwa kupigwa huku mlinzi wake, Bw. Michael akifungwa kamba na kutupiwa kwenye shimo la taka hadi majambazi hayo yalipoondoka na kuokolewa na askari polisi waliofika kwenye eneo hilo.

Alisema, majambazi hayo ambayo yanasadikiwa kufikia zaidi ya 10 walikuwa na silaa mbalimbali yakiwemo mapanga, marungu na bunduki na walivamia makazi ya viongozi hao na kufanikiwa kupora fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni tano na kutokomea nazo kusikojulikana.

“Kabla hawajazichukuwa fedha hizo walipambana na walinzi waliokuwa wakiwalinda, lakini walizidiwa nguvu na ndipo majambazi hayo yalimfunga kamba mlinzi mmoja na mwingine kumjeruhi kwa panga kichwani,” alisema Bw. Mwakajinga.

Kaimu Kamanda huyo alisema katika tukio hilo hakuna mtu ambaye amekamatwa hadi sasa na kwamba askari wanaendelea na kazi ya kuyasaka majambazi hayo ili yaweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Baadhi ya wananchi wanaodai waliweza kushuhudia sakata hilo lakini walishindwa kujitokeza kutoa msaada kutokana na majambazi hayo kufyatua risasi mbili hewani ambapo yalielekea kwenye makazi ya viongozi hao wakiwa kwenye gari moja aina ya Toyota 'Pick Up'.

No comments:

Post a Comment