Na Benedict Kaguo, Dodoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, imeibua ufisadi mpya wa utoroshaji wanyama na ugawaji wa vitalu vya uwindaji unaodaiwa kufanywa na maofisa wa Wizara wa Maliasili na Utalii, kinyume na sheria.
Hayo yalibainishwa Bungeni jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw.
James Lembeli, wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha Aprili, mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu ambapo Kamati hiyo imeitaka serikali kuwawajibisha waliohusika na tuhuma hizo zenye kulifedhesha Taifa.
Alisema kamati hiyo imebaini kuwa wizara ya maliasili na utalii Julai 19, mwaka juzi ilitoa kibali kilichosainiwa na B.M.C.M. Midala kwa niaba ya Katibu Mkuu kwa serikali ya jiji la Karachi kuruhusu usafirishaji wa twiga wawili,viboko wawili,kudu wawili na swala wanne kwa kibali cha ukamataji namba GD/R.20/2/87 cha Januari 27,mwaka juzi.
Bw. Lembeli, alisema mchakato wa ugawaji vitalu vya uwindaji uligubikwa na dosari kadhaa ikiwamo waziri kutangaza majina ya waliopatiwa vitalu bila kuonesha ni vitalu vipi wamepewa .
Alisema baadhi ya kampuni zilipewa vitalu kinyume na sheria na ushauri wa kamati ya kumshauri waziri kulingana na sifa na vigezo ikiwamo makampuni matatu; Mwanauta and company Ltd, Said Kawawa Hunting Ltd na Malagalasi Hunting Safaris Ltd kugawiwa vitalu bila kuwa na sifa zinazostahili
“Kamati pia ilibani kampuni 16 ziligawiwa vitalu ambavyo havikuombwa na kwamba vingi vya vitalu hivyo vikiwa daraja la kwanza na la pili wakati kulikuwa na kampuni za kizalendo zilizokuwa na vigezo, dosari hizi ziliathiri dhana ya uwazi na utawala bora, na kuashiria kuwapo kwa rushwa katika zoezi hilo na hivyo kusababisha malalamiko makubwa kutoka kwa waombaji,” alisema Bw Lembeli.
Alisema kuwa kamati ya Bunge inapendekeza kwamba Bunge liitake Serikali kumwajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige kwa kutengeneza mazingira ya rushwa pamoja na hatua ya kuzinyang’anya kampuni 16 vitalu zilizotolewa na Mwenyekiti huyo
ambaye pia ni Mbunge wa Kahama (CCM) alisema kuwa dhana ya utawala bora bado haijatekelezwa na wizara hiyo hasa kwa kuendelea kuwa mgawaji wa maeneo ya ugawaji wa vitalu ya uwindaji badala ya kuwa na mamlaka nyingine inatekeleza jambo hilo kisheria ili kuondoa hali ya sintofahamu inayojitokeza kwa sasa.
Kamati hiyo ilipendekeza bunge liagize Serikali kuwachukulia hatua kali za kinidhamu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Ledislaus Komba ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda na M. Madehele na wale wote waliohusika na utoaji wa vibali hivyo.
Aliongeza kuwa wizara ilitoa kibali cha kukamata wanyama kwa kampuni ya Jungle International wakati kwa mujibu wa taarifa za Msajili wa Makampuni (BRELA), kampuni hiyo haipo kihalali na wala haikupeleka maombi ya kupewa wanyama hao.
Alisema uchunguzi wa kamati ulibaini kuwa kibali alichopewa Kampuni ya Jungle International kilielezea ukamataji wa wanyama kufanyika katika wilaya za Longido, Simanjiro na Monduli, jambo ambalo ni kinyume na kanuni, kwani kibali cha ukamataji wanyama ni lazima kiainishe wilaya moja itakayohusika na ukamataji.
“Spika, kampuni ya Jungle si kampuni halali ya kuendesha biashara ya wanyamapori, kwani Desemba 28, 2001 ilibadili jina na shughuli zake na kwa sasa imesajiliwa kwa jina la Jungle Auctioneers & Brokers Company ambayo inafanya shughuli za udalali,”alisema.
Wakichangia taarifa hiyo wabunge walionesha kuchoshwa na ufisadi unaondelea nchini na kutaka hatua zaidi dhidi ya wahusika zichukuliwe haraka kuinusuru nchi.
Mbunge wa Vunjo,Bw Augustine Mrema (TLP),alisema kutokana na hali inayoendelea sasa serikalini ndio sababu shinikizo la kuwataka
mawaziri hao kujiuzulu kutokana na kuendelea kuihujumu nchi kila CAG
anapowasilisha taarifa yake..
Alisema viongozi wa CCM ndio wanaiangusha serikali yao kwani ni jambo la kushangaza kuona kampuni inapatiwa vibali bila kuomba
"Jamani hii ni nchi ni ya aina gani, ni kitu gani mnafanya?tuwaelewaje? hivi mnatuona wapinzani ni nyanya mbichi?...Mheshimiwa Spika funga mlango tushikane mashati, hapa ” alisema. Bw. Mrema
Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya Mjini,Bw Joseph Mbilinyi, alisema taifa lipoteza fedha nyingi kutokana na uzembe wa mawaziri na kuhoji wanyama kama twiga waliosafirishwa walitumia usafiri gani na kueleza kuwa kimbunga cha kuwang’oa mawaziri.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema mawaziri waogomakujiuzulu ni lazima wajiuzulu, kwani kitakachofuata ni tsumani katika suala hilo.
Alisema ni mambo ya kushangaza kila mwaka yanazungumza masuala hayohayo, lakini hakuna kinachobadilika na kuongeza kuwa vizazi vijavyo vitakuja kuwalaumu.
Ndugu Watanzania,
ReplyDeleteWakati umefika wa kupiga kura ya kutokuwa na IMANI na rais wetu - ni kwanini hataki kuwafuta kazi hao mawaziri wabovu?
Ushauri wa bure - wafukuze kazi haraka iwezekanavyo ili ulinde heshima yako na ya watanzania wote - ili muda wako wa utawala ukiisha, umpumzike kwa amani na heshima - usije ukawa kama rais wetu wa awali - kila anapopita anazomewa - je unataka hayo yakufike ndugu mheshimiwa?
Heshima na uadilifu ni vitu muhumi sana katika maisha ya mwanadamu mara tu vinapokutoka ni vigumu kuvirudisha.
Tutendee haki watanzania wenzako - usiache tukajuta kwanini tulikuchagu!!!
Rochas
Zanzibar