02 May 2012

AND1 yainyuka Dar All Stars 123-71

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya mpira wa kikapu ya AND1, kutoka nchini Marekani juzi iliinyuka timu ya Dar All Stars ya Dar es Salaam vikapu 123-71 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, iliyochezwa kwenye Uwanja wa ndani Taifa, Dar es Salaam.

Nyota hao nane ambao wanakipiga Marekani kwenye timu za mtaani walitua nchini Jumatano wiki iliyopita kwenye ziara ya siku tano katika Mikoa ya Mwanza, Arusha na Dar es Salaam ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Vinywaji baridi ya Coca-Cola kupitia kinywaji cha Sprite.

Katika mechi juzi mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko timu ya AND1, ilikuwa inaongoza kwa vikapu 64 huku Dar all Stars wakiwa na vikapu 23.

Nyota waliokuwa kivutio kwa mashabiki wa kikapu ni pamoja na Justine Fly, Paul Otim, High Rizer, Pharacist Davis, Lacue Brandon, Denis Chism, Philip Champion na Hot Sarce huku nyota wa Dar all Stars wakiwa wanawakilishwa na Juma Kisokcy, Frank Kusiga, Gerad Baru, Gilbert Batungi, Adamu Jegame, Fidelis Sunday, Sylivian Yunzu na Bernad Mageni.

Naye Meneja Mauzo wa Coca-Cola Tanzania, Demeji Olaniyan aliwapongeza wachezaji wa AND1 kwa ziara yao kwa mara nyingine nchini kwani imekuwa chachu kubwa kwa mpira wa kikapu kwa kuwahamasisha vijana kukuza mchezo huo.

Aliongeza kuwa kila mtu anajua uwezo binafisi walionao wachezajin wa AND1 kwa kasi na nguvu waliokuwa nayo kwenye manjonjo wanapokuwa uwanjani, kitu kinachowafanya wajulikane Dunia nzima kwa uwezo wao.

Pia alisema kwa sasa ni mara ya pili kwa kinywaji chao cha Sprite kwa kudhamini mechi za kirafiki kama hizo na kukiri kupata ushirikiano wa moja kwa moja kutoka kwa viongozi wa Chama cha Mpira Kikapu Tanzania (TBF), vyombo vya habari pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.




No comments:

Post a Comment