24 April 2012

JK aungana na vingozi wakuu kumzika Mutharika


Na Eckland Mwaffisi, Blantyre, Malawi

RAIS Jakaya Kikwete, jana aliungana na viongozi mbalimbali wa Afrika na Jumuiya za Ulaya kushiriki mazishi ya aliyekuwa Rais wa Malawi, marehemu Profesa Bingu wa Mutharika.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na idadi kubwa ya watu kutoka maeneo mbalimbali nchini hapa akiongozwa na Rais wa nchi hiyo, Bi. Joyce Banda.
Viongozi hao walitoa heshma za mwisho nyumbani wa marehemu Mutharika na baadae kushiriki 
ibada iliyofanyika  jirani na eneo alilozikiwa.


Mazishi hayo yamefanyika shambani kwake Ndata, kilometa 40 kusini mwa Blantyre, Wilaya ya Thloyo.


Maraisi walioshiriki mazishi hayo ni pamoja na Rais wa Kenya Bw. Mwai Kibaki, Rais wa Zimbabwe, Bw. Robert Mugabe, Rais wa Namibia Bw. Hithikepunye Pohamba na Rais wa Msumbiji Bw. Armando Guebuza.

Viongozi wengine ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini Bi.Kgalema Montlante na Waziri Mkuu wa Angola.

Tangu kiongozi huyo afariki asubuhi ya Aprili 5 mwaka huu, vyombo mbalimbali vya habari nchini hapa vimekuwa vikiripoti utata wa kifo hicho.

Utata huo unatokana na mazingira ya kifo chake ambacho kilishuhudiwa na mbunge wa Lilongwe Kusini Mashariki, Bi. Agness Penemulungu.

Baada ya madakatri kuthibitisha kifo hicho, Bi. Penemulungu alishikiliwa na vyombo vya usalama nchini hapa lakini walimuachia baada ya kumuhoji.

Kiu ya wanahabari nchini hapa ni kusikia kauli ya Bi. Penemulungu kuhusu mazingira ya kifo hicho ili kumaliza utata uliopo lakini hadi sasa, hajawa tayari kuzungumza na waandishi.

Mwili wa Mutharika ulizikwa jirani na kaburi la mke wake wa kwanza marehemu Esther ambaye alifariki mwaka 2007. katika mazishi hayo alipigiwa mizinga 21.

No comments:

Post a Comment