UPO msemo wa Kiswahili
ulizoeleka kuwa 'lisemwalo lipo
na kama halipo linakuja'.
Msemo huo leo baadhi ya
watumiaji wa Kiswahili hawautilii mkazo
kwa madai kuwa, kuna uwezekano wa
kuzushwa hata jambo ambalo halipo
hivyo kupoteza utafiti wa uhalisia kwa kile
ambacho kinawezekana kipo.
Hata hivyo katika Sheria ya Usalama wa
raia ndani ya Jeshi la Polisi upo utaratibu
wa kuhakikisha kuwa jeshi hilo linafanyia
kazi taarifa au fununu zinazolenga uhalifu
ama jambo lolote la uvunjifu wa sheria na
taratibu ya usalama wa raia na mali zao.
Jambo hili mara nyingi husaidia jeshi la
polisi kuzuia vitendo vya uhalifu kabla ya
kutokea la sivyo tungeshuhudia madhara
makubwa zaidi kama polisi ingekuwa
inasubiri mpaka tukio halisi lionekane.
Katika kampeni mbalimbali zipo
tuhuma na kashfa ambazo baadhi ya
wanasiasa wamekuwa wakirushia baadhi
ya wagombea wa uongozi kupitia vyama
mbalimbali vya siasa lakini hazifanyiwi
kazi.
Tuhuma hizo hukanushwa juujuu na
walalamikiwa na kuwafumba macho
wananchi ili kuwachagua viongozi wabaya
ambao matokeo ni rasilimali ya nchi
kuwafaidisha viongozi wenyewe na
marafiki zao.
Propaganda hizi ambazo baadhi zao
hazina ukweli wowote zimejaa katika
vichwa vya watu na kusababisha chuki,
hasira na ulipaji wa visasi.
Wanasiasa katika hotuba zao wameacha
kuwaeleza watanzania sera walizoandika
katika vitabu vyao wakati wanaomba
usajili badala yake wamegeukia kashfa,
matusi, fujo na lawama dhidi ya wenzao
mambo haya sio salama kwa mustakabali
wa taifa letu.
Siwezi kusahau jinsi siasa chafu
ilivyotumika mwaka 2005 ambapo
baadhi ya watu wazuri walioaminiwa
kuwa wangekuwa viongozi bora
walivyochafuliwa kwa kashfa na tuhuma
ambazo naamini sehemu kubwa zilikuwa
si za kweli.
Wakati huo huo baadhi ya wagombea
ambao Watanzania walifahamu kasoro zao
katika uongozi wakisafishwa huku kashfa
na tuhuma zao zikionekana kuwa ni uzushi
ambapo baada ya kutakatishwa kwa nje
walipigiwa kura na kupewa nyadhifa hizo
ambazo leo tunashuhudia matokeo yake.
Vyombo vingi vya habari vilishiriki
katika propaganda hizo kwa vile tu
baadhi ya wahariri na waandishi wa
habari waliahidiwa nafasi nzuri baada ya
kusafisha njia.
Tukumbuke kuwa, kupitia propaganda
zenye lengo la kuwagawa wananchi katika
makundi kwa kufanya ukweli kuwa uongo
na uongo kuwa kweli zinazoenezwa na
vyombo vya habari zimeingiza nchi
mbalimbali katika mapigano ya wenyewe
kwa wenyewe.
Ni propaganda za kichochezi za
wanasiasa zilizoenezwa na vyombo vya
habari zilisababisha nchi ya Rwanda
kuingia katika vita na mauaji ya wenyewe
kwa wenyewe kwa lengo la kulipizana
kisasi japo wapo wanaodai ni bora hali
hiyo itukumbe Tanzania kwa kuwa ndio
njia ya ukombozi.
Sitaki nizungumzie ya Rwanda lakini
vyombo hivyo ambavyo huwasafisha
baadhi ya wagombea wakati wa kampeni
kutumia propaganda ya wanasiasa ndivyo
vinakuwa wa kwanza kuwalaumu viongozi
hao wanapodhihirisha udhaifu wao kipindi
cha uongozi wao.
Kuna orodha ndefu ya viongozi wa
kisiasa ambao wamewahi kutuhumiwa
kwa makosa mbalimbali lakini tuhuma hizo ziliishia
kiholela bila kueleza madhara yake kwa wahusika
wala kwa wananchi wenyewe ili kuzuia zaidi
yanayoweza kujitokeza baadaye.
Hatuwezi kusahau kashfa zilizotajwa kwa baadhi
ya wanasiasa wakongwe katika nchi hii kama Rais
mstaafu Bw. Benjamin William Mkapa, Dkt.Salim
Mohamed Salim, waziri Mkuu mstaafu Bw. Fedrick
Sumaye, aliyekuwa Waziri mkuu Bw. Edward
Lowasa na wengineo.
Baadhi ya viongozi hawa walikashfiwa kwa
tuhuma mbalimbali ambapo kwa rais Mkapa mbali
na kashfa ya kuuza kiholela rasilimali ya taifa
kipindi cha utawala wake lakini hivi karibuni Vicent
Nyerere alimtuhumu kuwa alichangia kifo cha Baba
wa Taifa Mwl. Julius Nyerere.
Tunajua katiba yetu bado inamlinda rais
asishtakiwe hata baada ya kumaliza utawala wake
lakini ikumbukwe kuwa Katiba si msaafu, ipo siku
vizazi vijavyo vitahitaji ukweli huo baada ya katiba
kubadilishwa ni vyema ukweli uwe wazi sasa.
Kwa upande wake Dkt. Salim Mohamed Salim
katika Kampeni ya uchaguzi mkuu mwaka 2005
akiwa miongoni mwa waliokuwa wakiwania kiti
cha urais kupitia CCM aliibuliwa tuhuma kuwa
hakuwa mzaliwa na raia wa Tanzania wakati sisi
tulijua alikuwa raia na kushika nyadhifa mbalimbali
za uongozi nchini.
Isitoshe wote kwa wakati tofauti Bw. Sumaye na
Bw. Lowasa walituhumiwa kuhusika na ufisadi na
kuhodhi mali ya umma kinyume na utaratibu lakini
yote Msajili wa vyama vya siasa, NEC wala jeshi
la polisi halikuchukua hatua yoyote dhidi ya vyama
vya siasa au watu waliotoa kashfa hizo.
Zipo pia kashfa zinazotajwa hata kwa baadhi
ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao nao
wanaomba ridhaa kuongoza nchi wathibitishwe
kwamba wao ni wasafi katika historia ya maisha
yao kiasi cha kuweza kuongoza nchi kwa misingi
ya kimaadili.
Zipo baadhi ya kashfa na tuhuma zinazoelekezwa
kwa Dkt. Willibrod Slaa kwamba zilichangia yeye
kuacha kumtumikia Mungu na kuingia katika siasa
ni vyema tuhuma hizo zitolewe maelezo ya kutosha
kabla ya kupewa wadhifa wa kuongoza nchi.
Ni chombo kipi kimeshughulikia kashfa hizo
na kutoa ukweli halisi kwa umma wa watanzania
ikizingatiwa kuwa hao ni wanasiasa wakongwe
ambao wamewahi kushika nyadhifa kubwa za
uongozi ya serikali ya Tanzania.
Isitoshe kashfa, matusi na vitendo vya vurugu
bado vinatawala katika kampeni za wanasiasa
kuanzia ngazi za vitongoji kwa wenyeviti wa serikali
za mitaa, vijiji, madiwani na wabunge.
Kashfa hizi ambazo vyombo husika hazitaki kutoa
ufafanuzi wa kina kwa watanzania ndilo bomu
kubwa linasubiri kuvuruga amani ya watanzania.
Ni ukweli usiopingika kuwa wanasiasa wanapenda
kutumia uchochezi na vurugu kujipatia madaraka
bila kujali maisha ya wananchi wao wanyonge .
Tunaomba vyombo vya usalama wa nchi
yetu itoe majibu kwa watanzania kuhusu hatua
zilizochukuliwa kwa watu hao na kama tuhuma hizo
ni za uongo pia ielezwe hatua zilizochukuliwa kwa
vyanzo vya habari hizo.
Vyama vya siasa huibuka na kupita lakini
utanzania hubaki vizazi hata vizazi hivyo vyombo
vya usalama ikiwa ni pamoja na polisi, mahakama
na usalama wa taifa vihakikishe kuwa amani,
umoja na mshikamo ambazo ndizo nguvu ya utaifa
hazivurugwi na wanasiasa.
Ninaeleza hapa ni kuwa, madhara yatakayoikumba
jamii ya Watanzania katika dhana nzima ya uongozi
wa taifa pale jamii inaposhindwa kubaini ukweli juu
ya maisha halisi ya viongozi wanaowachagua badala
yake kufanyia kazi ushabiki, rushwa na urafiki.
Katika wakati huu wa vyama vya siasa vya
upinzani wapo wanasiasa ambao aidha walifukuzwa
katika vyama vyao vya awali kutokana na kashfa
na uvunjifu wa maadili katika kuwania madaraka .
Lakini hao ndio wanaojisafisha ndani ya vyama
vyao vipya na kuonekana wasafi ili wapewe
madaraka licha ya tuhuma zao na kashfa za awali.
Mbaya zaidi ni pale ambapo sehemu kubwa ya
jamii haitaki kufumbua macho kwa kutaka ukweli
juu ya kashfa hizo badala yake wanakalia ushabiki na
kukubali kumpa ridhaa mtu mchafu ambaye baadaye
huchafua serikali yao.
Jeshi la polisi lisiogope kuwachukulia hatua
viongozi wa kisiasa ambao hutumia nafasi zao
kuvuruga amani na utulivu wa wananchi kwa vile
wanapendwa na wengi hivyo hutumia uwingi wa
ushabiki kuhalalisha makosa yao.
wATYACHUWAJE HATUA WAKATI SIYO WASAFI?????????????
ReplyDelete