Na Said Hauni, Lindi
WANAFUNZI wapatao 326 sawa
na asilimia 22 kati ya 1,605,
waliochaguliwa kujiunga na
masomo ya sekondari mwaka
huu katika Halmashauri ya Lindi mkoani
Lindi bado hawajaripoti kwenye shule
walizopangiwa.
Imebainika kuwa hali hiyo inatokana na
sababu mbalimbali zikiwemo za uwezo
mdogo wa kiuchumi kwa baadhi ya wazazi.
Takwimu hizo zilitolewa na Ofisa Elimu
Shule za Sekondari katika halmashauri hiyo,
Bw. James Milanzi hivi karibuni wakati
akizungumza na mwandishi wa habari hizi
wilayani humo.
Bw. Milanzi alisema wanafunzi hao
wakiwemo wavulana 208 na wasichana 117
bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa
hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Februari
mwaka huu.
Alisema, tangu shule zilipofunguliwa
zikiwemo za sekondari zilipofunguliwa
ni wanafunzi wapatao 1,475 wakiwemo
wavulana 902 na wasichana 673 ndio
waliokwisha ripoti kuendelea na masomo yao
ya kidato cha kwanza msimu huu.
Aidha, akitaja mikakati itakayosaidia
kuwafanya wanafunzi hao 326 kuripoti
shuleni, Bw. Milanzi alisema ni pamoja
na kuwafikisha mahakamani wazazi na
walezi wote ambao vijana wao hawataripoti
katika shule walizopangiwa kama
walivyokubaliana.
"Kama watoto wao hawahudhurii shuleni
basi sheria itachukuwa mkondo wake wa
kuwafikisha mahakamani wazazi na walezi
wote kama tulivyokubaliana, kwani tayari
tumeshawekeana mikataba," alisema Bw.
Milanzi.
Bw. Milanzi alisema kuna athari nyingi
zinazowapata wanafunzi wanaochelewa
kuripoti shuleni, ikiwa ni pamoja na
kuachwa nyuma katika masomo na wenzao
waliotangulia hivyo kuwafanya vijana hao
kuhesabiwa kuwa ni watoro shuleni na
hatimaye kujiunga kwenye vikundi vya
uhalifu.
Ofisa elimu huyo aliongeza kuwa wapo
baadhi ya wazazi na walezi, kwa kiasi
kikubwa wamekuwa wanachangia watoto
wao wasiende shule lakini halmashauri
imeweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha
wazazi kuwapeleka watoto wao hata kama
hawana ada au sare za shule, kuendelea kutoa
nafasi ya kujitafuta wakiwa ndani ya darasa
na siyo nje.
"Mfano mzazi anaweza kulipa ada ya
shule kwa kutoa nusu nusu kama shilingi
5,000 au sh. 10,000 , na walimu wako tayari
kupokea fedha hizo mpaka pale mzazi
akatakapokamilisha ada yote ya sh. 20,000
pamoja na sare za shule," alisema Bw.
Milanzi.
Akizungumzia upungufu wa walimu
unazoikabili shule nyingi za sekondari
ikiwemo za kutwa ofisa huyo alisema, suala
hilo kwa sasa linaendelea kupungua kutokana
na Serikali kuleta walimu 48 kati ya walimu
63 waliopangwa katika Halmashauri ya
Wilaya ya Lindi.
Hata hivyo, Bw. Milanzi alisema, bado
kuna tatizo kubwa la ukosefu wa walimu wa
masomo ya sayansi, kwani kati ya walimu
hao 48 walioletwa ni walimu wawili tu ndiyo
wenye taaluma ya masomo ya sayansi na
hivyo kusababisha shule zingine kutoipata elimu hiyo.
No comments:
Post a Comment