UTASHI wa kusaidia
ama kujitolea katika
shughuli za kijamii
hasa zinazolenga
kuharakisha maendeleo tafiti
zinabainisha kuwa ni moja
wapo ya hatua madhubuti katika
kuendeleza uchumi endelevu.
Mbali na hayo uwezeshaji huo
unaweza kufanikisha uchumi
huo katika jamii husika ikawa
imejengewa mazingira mazuri
ambayo kwa misingi ya kanuni
na taratibu unaweza kubainisha
kuwa ni mafanikio yenye tija.
Ili kufanikisha jitihada hizo
mbali na nguvu kazi kutoka kwa
wananchi pia suala la fedha ni
la msingi kwa kuwa mahitaji
mengi yanahitaji kununuliwa.
S h i l i n g i b i l i o n i m o j a
inahitajika kwa ajili ya
kuimarisha miundombinu ya
elimu katika Kata ya Kipawa
iliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar
es Salaam ambayo imeonekana
kuchakaa kiasi cha kufanya
wanafunzi kushindwa kufanya
vizuri katika mitihani yao ya
mwisho.
Ni dhairi kuwa mahitaji ya
fedha hizo yametokana na utafiti
uliofanywa na Diwani wa kata
hiyo, Bi. Bonna Kaluwa juu ya
hali halisi ya elimu katika kata na
nini kinahitajika kufanyika hili
kuboresha elimu katika kata hiyo.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa
shule nyingi nchini zinakabiliwa na
ubovu wa miundombinu ikiwemo
ukosefu wa vitendea kazi, hivyo
anapotokea mtu au mdau ambaye
anafanikiwa kubuni njia za kuyafikia
malengo ili kuifanya elimu ya
Tanzania kuwa bora anapaswa
kuungwa mkono kwa asilimia 100.
Mbali na hayo kwa kuona hilo
Diwani huyo aliamua kufanya mradi
shirikishi unaokwenda kwa jina la
'Mazingira Bora kwa Elimu Bora'
ambao una lengo la kuwashirikisha
wadau mbalimbali wa maendeleo
waliopo ndani ya Kipawa na nje ya
kata hiyo kuijengea sekta ya elimu
uwezo.
Bi. Kaluwa ambaye ameonekana
kuwa tumaini jema kwa wakazi wa
Kipawa na watu wengi kumpongeza
kuwa ndiye Diwani pekee
mwanamke ambaye ameweza kuwa
na uthubutu wa kubuni mradi ambao
unahusika kuwagusa wananchi moja
kwa moja.
Hivi karibuni Diwani huyo
ambaye ameonekana kuwa na kiu ya
kumaliza tatizo la elimu katika kata
hiyo alisema, anaamini kuwa elimu
ndio chachu kubwa ya maendeleo
katika ulimwengu wa leo wa sayansi
na teknolojia.
Pia anasema, ameweza kutumia
marafiki wa karibu ili kuhakikisha
kuwa anapiga hatua katika masuala
ya kusaidia elimu katika kata hiyo
ambayo imeonekana kuwa na usugu
wa miundombinu ya elimu.
Kwa mujibu wa, Bi. Kaluwa
kwa kushirikiana na Manispaa ya
Ilala, waliweza kuandaa matembezi
ya hisani kwa ajili ya kuchangia
madawati ambayo yanalenga
kuzisaidia shule zilizopo katika
kata hiyo.
Anasema, mara baada ya kupata
wazo hilo ambalo ni jema katika
jamii aliamua kuwashirikisha
watendaji mabalimbali waliopo
katika Manispaa ya Ilala na
kumuunga mkono katika ufanikishaji
wa matembezi hayo.
Diwani huyo anasema katika
matembezi hayo waliweza
kukusanya jumla ya kiasi cha
sh. milioni 18 kutoka kwa watu
mbalimbali ambao waliudhuria
matembezi hayo kama ishara ya
ufunguzi wa uchangiaji elimu katika
kata hiyo.
Bi. Kaluwa aneleza kuwa kata
yake inakabiliwa na changamoto
mbalimbali lakini kwa sasa
ameamua kuanza na sekta ya
elimu kwa kuboresha madarasa,
vyoo na hupatikanaji wa madawati
lengo likiwa ni kuhakikisha kila
mwanafunzi anapata elimu bora
katika mazingira bora.
Anasema, anatarajia kukusanya
sh. bilioni moja kutoka kwa wahisani
mbalimbali na watu ambao wana kiu
ya elimu katika kata hiyo ya Kipawa
na uchungu wa kizazi cha sasa na
kijacho.
Hivyo aliwaomba wahisani
na wananchi kujitokeza kwa
wingi katika hafla ya uchangiaji
itakayofanyika Mei 19, mwaka huu
katika Hoteli ya Kempisk jijini Dar
es Salaam ili kuweza kuchangia
hupatikanaji wa madawati.
Anaeleza kuwa kwa sasa kata hiyo
ina upungufu wa madawati zaidi
ya 3,000 katika shule zote zilizopo
wakati ambao wanafunzi wanakaa
chini.
Bi.Kaluwa anasema ana uchungu
na maendeleo ya wananchi wake
hivyo anachokifanya ni uwajibikaji
na anatekeleza wajibu wake kama
kiongozi.
Anasema, matembezi hayo
yaliyofadhiliwa na Home Shopping
Center yalifanyika awali kabla ya
awamu ya pili inayokuja Mei mwaka
huu, ambapo yalifanyika Machi 17,
mwaka huu kuanzia saa 12 asubuhi
katika Shule ya Msingi Minazi
Mirefu na mgeni rasmi alikuwa mke
wa Rais Mama Salma Kikwete.
Bi. Kaluwa ambaye ameonesha
kuwa chachu ya maendeleo katika
sekta ya elimu hapa nchini na
hata mfano wa kuigwa na kata
nyingine aliweza kupongezwa na
Mbunge wa Jimbo la Segerea, Dkt.
Makongoro Mahanga kwa kubuni
mikakati ya kuboresha elimu hasa
kwa kuchangia madawati ambayo
yamekuwa ni kero kubwa.
Kumekuwepo na juhudi za
kuongeza madawati na mimi
kupitia Mfuko wa Jimbo nimekuwa
nikitenga fedha kwa ajili hiyo, kwa
sasa tuna upungufu wa madawati
kwa asilimia 40 na kila kata imekuwa
ikibuni mbinu na taratibu zake ili
kuhakikisha tatizo hili linakwisha,
alisema Dkt.Mahanga.
Dkt. Mahanaga ambaye aliitaka
jamii kushirikia kikamilifu katika
kuchangia maendeleo yao kwa kuwa
Serikali pekee haiwezi ambapo pia
aliwasihi wananchi wenye uchungu
na maendeleo ya elimu kujitokeza
katika matembezi hayo na kuchangia
chochote.
Katika kuchangia maendeleo
ya Kipawa Mama Salma Kikwete
aliwataka wananchi wa Kipawa
kulinda miundombinu iliyowekwa
na serikali pamoja na wadau wengine
kwani kila mtu anahisa katika elimu.
Mama Kikwete alisema, suala
la ujenzi wa madawati ni la kila
mwananchi hivyo ni vema kila mtu
akajitoa kwa moyo mmoja katika
kufanikisha kiasi cha shilingi bilioni
moja zinazohitajika ili kutatua
matatizo ya Kipawa.
Hivyo ni wajibu wa kila
mwananchi kuhakikisha kuwa
anahisaidia Serikali katika
mapambano dhidi ya ujinga na
kuacha malalamiko kuwa serikali
aiwatimizii mahitaji yao, alisema
Mama Salma Kikwete.
Alisema, jambo muhimu ni
kuangalia ni mtu gani anapewa
nafasi ya kusimamia masuala ya
elimu na ni wajibu wa kila mtu
kujisimamia ili kuhakikisha kuwa
vifaa vya shule vinatunzwa.
Kwa upande wake Diwani wa
Kata ya Kipawa, Bi. Bonna Kaluwa
alihaidi kuwa yeye kama kiongozi
kijana mwenye chachu ya maendeleo
kwa Watanzania atahahikikisha
anahamasisha wananchi waweze
kuchangia katika zoezi hilo hili
miundombinu ya elumu iweze
kuimarika kufikia mwishoni mwa
mwaka 2012.
Aliongeza kuwa, matatizo
yanayowakabili katika shule za
Kipawa ni pamoja na upungufu wa
matundu vya vyoo, ofisi za walimu,
stoo, maabara, vyumba vya maktaba
na majengo ya utawala ambayo
yameonekana kuchoka kabisa.
Sambamba na hayo anasema,
mbali na hayo kuna upungufu wa
maji, uzio na ukosefu wa umeme
katika shule za msingi Majani ya
Chai, Mogo, Karakata na Sekondari
ya Majani ya Chai.
Hata hivyo Diwani huyo anaeleza
kwamba katika Kata ya Kipawa
kuna shule za msingi ambazo zina
wanafunzi 7,919 na kati ya hao
wavulana ni 3997 huku wasichana
wakiwa 3,922.
"Wanafunzi wenye ulemavu wa
akili ni 52 na wavulana 33 ambapo
wasichana 19 wakati ambao shule za
sekondari ni mbili zenye wanafunzi
2,171. Huku wavulana wakiwa 1,146
na wasichana 1,025," anasema.
No comments:
Post a Comment