28 March 2012

Wajasiliamali kuendelezwa

Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro
Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kimesema kitaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali hapa nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawezesha kuingia katika soko la ushindani katika biashara na kukuza mitaji yao.
Meneja wa TIC Kanda ya Kaskazini, Bw. Clement William, aliyasema hayo mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku sita ya wajasiriamali wa kati na wadogo yaliyolenga kuwaunganisha na wawekezaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi.

“Ukitaka kujenga uchumi imara katika nchi ni vema ukaanza kujenga kada ya wajasiriamali wadogo ili waweze kuwa na uwezo wa kufanya biashara na wawekezaji wakubwa, huu ndio msingi mkubwa katika suala la uwekezaji popote pale,” alisema Bw Clement.

Alisema hii ni mara ya kwanza kwanza kwa Kituo cha uwekezaji kutoa mafunzo ya aina hiyo katika kanda ya kaskazini, na kusisitiza kuwa huo ni mwanzo tu wa safari yao ya kuwajenga uwezo watanzania hao waweze kukua ndani na nje ya nchi.

“Programu hizi zitaendelea kutolewa pale inapobidi ili kuweza kuwajenga wananchi kuwa na uwezo wa kukuza mitaji yao,” alisema, na kuongeza kwamba ni vyema ukampa mtu mafunzo yatakayomjenga kuliko kumpa fedha ambazo atatumia siku chache na baadae atamaliza na kubaki pale pale alipo.

Aliongeza kuwa mikoa ya kanda ya Kaskazini ina wafanyabiashara wengi hivyo watajaribu kuangalia uwezekano wa kutoa mafunzo ya aina hii mara kwa mara ili kuwakumbusha wajibu wao wa kukuza mitaji yao na kuongeza pato la Taifa na kaya zao.

“Unapomjenga mjasiriamali kama huyu unampa nguvu ya kuongeza pato la Taifa pamoja na kipato katika kaya zao, hii inakuja pale anapolipa kodi kama mfanyabiashara aliyekamilika,” aliongeza Bw. Clement.


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Ruth Malisa, alisema kwa kufanya hivyo TIC inatoa fursa zaidi za ugavi, usambazaji na kuuza bidhaa na huduma zinazotengenezwa na wajasiriamali wenyewe.

“Ni imani yangu kuwa mafunzo kama haya ni mhimili wenye tija katika kukuza uchumi wetu katika nyakati hizi za utandawazi, hivyo ni muhimu kujiimarisha kielimu ndipo tuweze kumudu ushindani wa kibiashara,” alisema Bi. Malisa.

Aliongeza kuwa ni imani yake kuwa baada ya mafunzo hayo wajasiriamali hao wataweza kuweka mipango yao mizuri ya biashara, kukusanya taarifa, kubadili mitazamo hasi, kutunza mahesabu, kuandaa michanganuo ya kibiashara, kuhudumia wateja na watakuwa watu wakukopesheka katika mabenki mbalimbali.

Mmoja wa wajasiriamali waliohudhuria mafunzo hayo, Bw. Isaki Ara, aliipongeza TIC kwa kuwajali watanzania ambao wana mwamko wa kufanya biashara na wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya nchi ili na wao waweze kuwa wawekezaji wazuri katika nchi yao

“Napenda kutoa shukrani nyingi kwa kituo hiki kwa kutuletea mafunzo haya katika kanda yetu, hii itatusaidia kuweza kufahamu namna ya kufanya biashara na wawekezaji wakubwa na pia kuongeza utaalamu kupitia mafunzo mbalimbali, hivyo ni vema TIC ikaendelea kutujali,” alisema Isaki.

Mafunzo hayo yameandaliwa na TIC kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Biashara Duniani la Umoja wa Mataifa (UNCTAD).

No comments:

Post a Comment