28 March 2012

Mkuranga watakiwa kulipa zao la muhogo kipaumbele

Na Bahati Mohamed, aliyekuwa Pwani
WAKULIMA Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wamehamasishwa kujikita katika kilimo cha zao la muhogo ili kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo sambamba na kujihakikishia chakula cha uhakika.
Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Henry Clemens ambapo alisema njia pekee ya wananchi wake kutoka katika dimbwi la umaskini ni kujikita katika kilimo hasa zao la muhogo.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake, Bw. Clemens alisema wananchi wake lazima waongeze jitihada za kilimo hasa zao la muhogo kwani eneo hilo lina ardhi yenye rutuba inayokubali zao hilo.

"Wilaya imeamua kuchukua hatua za makusudi kuwahamasisha wananchi ili kuwekeza kwenye kilimo ili kuweza kukabiliana na ugumu wa maisha,"alisema Bw. Clemens.

Aliongeza kuwa wilaya hiyo imechukua hatua za kukusanya mbegu za muhogo kutoka nje ya Mkuranga na kuwaletea wanachi ili waweze kuzipanda katika mashamba yao ambapo usimamizi utakuwa chini ya wilaya hiyo.

Alisema, wilaya imeweza kuliangalia zao hilo la muhogo na kuliona linaweza kuwa ndiyo mkombozi kwa Wanamkuranga hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika ipasavyo.

"Nachoweza kusema wanachi wangu waache uvivu na kukubaliana na mpango huu wa wilaya wa kuwaharakishia maendeleo kupitia zao hili na lile la korosho," alisema Bw. Clemens.

Aliongeza kuwa, baada ya kuhamasisha katika upande wa zao la korosho sasa wanageukia upande wa muhogo na lengo ni kutaka kuona wilaya hiyo wananchi hawafi njaa.

No comments:

Post a Comment