Na Mwajabu Kigaza, Kigoma
WANANCHI waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji wamejenga hofu ya usalama wa maisha yao kutokana na ongezeko la vibaka kufanya vitendo vya unyang’anyi wa kutumia silaha na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani mkoani hapa.
Wakizungumza na Majira mkoani hapa baadhi ya wananchi hao walisema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo vya uporaji vimesababisha wao kutofanya shughuli zao kwa amani.
Aidha, vitendo vinavyoendelea mkoani hapa kwa muda mrefu vimeonekana kuwa kero kwa wananchi ambapo wananchi wengi wemepata hasara ya kupokonywa mali kama fedha, simu, wengine kujeruhiwa na kupoteza maisha yao.
“Hatuna kimbilio lolote wananchi, tumekosa imani na Jeshi la Polisi, ikifika saa 12 watu wote wanarudi majumbani kwa kuhofia kupoteza maisha yao,” alisema mmoja wa wakazi hao.
Aidha, walisema kuwa maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na vibaka hao ni maeneo ya Mlole, Masanga, Nazareth, Kisangani na mtaa wa Lumumba Road ambapo katika maeneo hayo wapo watu ambao walivamiwa wakiwa njiani na wengine kuvunjiwa majumba yao.
Hata hivyo kwa upande wa baadhi ya maofisa wa polisi ambao hawakupenda kuandikwa majina yao gazetini walikiri kuwepo kwa vitendo hivyo na kusema kuwa hatua mbalimbali zinachukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanapata usalama wa kutosha.
Aidha, walisema kuwa baadhi ya watu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua za kiuchunguzi ambapo kuna baadhi yao ambao wamebainika na kufikishwa mahakamani na hatua hizo zinaendelea.
Awali baadhi ya wananchi walisema, hali kama hiyo ilishawahi kutokea mkoani hapa ambapo wananchi wengi walijeruhiwa na kupoteza mali zao mbalimbali na sasa imerejea tena.
No comments:
Post a Comment